Ezekieli 1:1-14
Ezekieli 1:1-14 NEN
Katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, wakati nilipokuwa miongoni mwa hao waliokuwa uhamishoni kando ya Mto Kebari, mbingu zilifunguka nami nikaona maono ya Mungu. Katika siku ya tano ya mwezi, ilikuwa mwaka wa tano wa kuhamishwa kwa Mfalme Yehayakini, neno la BWANA lilimjia Ezekieli kuhani, mwana wa Buzi, kando ya Mto Kebari, katika nchi ya Wakaldayo. Huko mkono wa BWANA ulikuwa juu yake. Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini, wingu kubwa sana pamoja likiwa na umeme wa radi likiwa limezungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama rangi ya manjano ya chuma kinapokuwa ndani ya moto. Katika ule moto kulikuwa na kitu kinachofanana na viumbe vinne vyenye uhai. Katika kuonekana kwake vilikuwa na umbo mfano wa mwanadamu, lakini kila kimoja kilikuwa na nyuso nne na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyooka, nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa, nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja, hawakugeuka walipokuwa wanatembea. Kuonekana kwa nyuso zao kulikuwa hivi: Kila mmoja wa wale wanne alikuwa na uso wa mwanadamu na kwa upande wa kulia kila mmoja alikuwa na uso wa simba, upande wa kushoto alikuwa na uso wa ngʼombe pia kila mmoja alikuwa na uso wa tai. Hivyo ndivyo zilivyokuwa nyuso zao. Mabawa yao yalikunjuliwa kuelekea juu, kila mmoja alikuwa na mabawa mawili ambayo kila moja liligusa bawa la mwenzake kila upande na mabawa mengine mawili yakifunika mwili wake. Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja. Popote roho alipotaka kwenda, ndipo walipokwenda pasipo kugeuka. Kuonekana kwa vile viumbe hai katikati kulikuwa kama makaa ya mawe yanayowaka au kama mienge. Moto ule ulikuwa ukienda mbele na nyuma katikati ya vile viumbe, ulikuwa na mwangaza mkali na katikati ya ule moto kulitoka kimulimuli kama umeme wa radi. Vile viumbe vilipiga mbio kwenda na kurudi, kama vimulimuli vya umeme wa radi.