Ezekieli 14:12-23
Ezekieli 14:12-23 NENO
Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema, “Mwanadamu, nchi ikinitenda dhambi kwa kutokuwa waaminifu nami nikaunyoosha mkono wangu dhidi yake ili kukatilia mbali upatikanaji wake wa chakula na kuipelekea njaa na kuua watu wake na wanyama wao, hata kama watu hawa watatu: Nuhu, Danieli na Ayubu wangekuwa ndani ya nchi hiyo, wangeweza kujiokoa hao wenyewe tu kwa uadilifu wao, asema Bwana Mungu Mwenyezi. “Au nikiwaachilia wanyama pori katika nchi hiyo nao wakaiacha bila watoto, nayo ikawa ukiwa hivi kwamba hakuna mtu apitaye kwa sababu ya wanyama pori, hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao peke yao wangeokolewa, lakini nchi ingekuwa ukiwa. “Au nikileta upanga dhidi ya nchi hiyo na kusema, ‘Upanga na upite katika nchi yote,’ nami nikaua watu wa nchi hiyo na wanyama wao, hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao wenyewe tu wangeokolewa. “Au nikipeleka tauni katika nchi hiyo na kumwaga ghadhabu yangu juu yake kupitia kumwaga damu, kuua watu wa nchi hiyo na wanyama wao, hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama Nuhu, Danieli na Ayubu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kumwokoa mwana wala binti. Wao wangeweza kujiokoa wenyewe tu kwa uadilifu wao. “Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Itakuwa vibaya kiasi gani nitakapopeleka dhidi ya Yerusalemu hukumu zangu nne za kutisha, yaani upanga, njaa, wanyama pori na tauni, ili kuua watu wake na wanyama wao! Lakini patakuwa na watakaookoka: wana wa kiume na wa kike watakaoletwa kutoka nchi hiyo. Watakuja kwenu, nanyi mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, mtafarijika kuhusu maafa niliyoleta juu ya Yerusalemu, kwa ajili ya maafa yale yote niliyoleta juu yake. Mtafarijika mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, kwani mtajua kuwa sikufanya lolote ndani yake bila sababu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”