Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 23:1-21

Ezekieli 23:1-21 NEN

Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, walikuwepo wanawake wawili, binti wa mama mmoja. Wakawa makahaba huko Misri, wakajitia kwenye ukahaba tangu ujana wao. Katika nchi ile vifua vyao vya ubikira vikakumbatiwa huko na wakapoteza ubikira wao. Mkubwa aliitwa Ohola na mdogo wake Oholiba. Walikuwa wangu nao wakazaa wavulana na msichana. Ohola ni Samaria, Oholiba ni Yerusalemu. “Ohola akajitia kwenye ukahaba alipokuwa bado ni wangu, akatamani sana wapenzi wake, mashujaa Waashuru, waliovaa nguo za buluu, watawala na majemadari, wote walikuwa wanaume vijana wa kuvutia, wapandao farasi. Akafanya ukahaba na wasomi wote wa Ashuru, na kujinajisi kwa sanamu zote za kila mwanaume aliyemtamani. Hakuacha ukahaba wake aliouanza huko Misri, wakati ambapo tangu ujana wake wanaume walilala naye, wakikumbatia kifua cha ubikira wake na kumwaga tamaa zao juu yake. “Kwa hiyo nilimtia mikononi mwa wapenzi wake, Waashuru, kwa kuwa ndio aliowatamani. Wakamvua nguo zake wakamwacha uchi, wakawachukua wanawe na binti zake, naye wakamuua kwa upanga. Akawa kitu cha kudharauliwa miongoni mwa wanawake na adhabu ikatolewa dhidi yake. “Oholiba dada yake aliliona jambo hili, lakini kwa tamaa zake na ukahaba wake, akaharibu tabia zake kuliko Ohola dada yake. Yeye naye aliwatamani Waashuru, watawala na majemadari, mashujaa waliovalia sare, wapandao farasi, wanaume vijana wote waliovutia. Nikaona kuwa yeye pia alijinajisi, wote wawili wakaelekea njia moja. “Lakini yeye akazidisha ukahaba wake. Akaona wanaume waliochorwa ukutani, picha za Wakaldayo waliovalia nguo nyekundu, wakiwa na mikanda viunoni mwao na vilemba vichwani mwao, wote walifanana na maafisa wa Babeli wapandao magari ya vita, wenyeji wa Ukaldayo. Mara tu alipowaona, aliwatamani, akatuma wajumbe kwao huko Ukaldayo. Ndipo hao Wababeli wakaja kwake kwenye kitanda cha mapenzi, nao katika tamaa zao wakamtia unajisi. Baada ya kutiwa unajisi, akawaacha kwa kuwachukia. Alipofanya ukahaba wake waziwazi na kuonyesha hadharani uchi wake, nilimwacha kwa kumchukia, kama vile nilivyokuwa nimemwacha dada yake. Lakini akazidisha zaidi ukahaba wake alipozikumbuka siku zake za ujana, alipokuwa kahaba huko Misri. Huko aliwatamani wapenzi wake, ambao viungo vyao vya uzazi ni kama vya punda, na kile kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi. Hivyo ulitamani uasherati wa ujana wako wakati ulipokuwa Misri, kifua chako kilipokumbatiwa, na walipokutomasa kwa sababu ya matiti yako machanga.