Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 23:1-21

Ezekieli 23:1-21 BHN

Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Palikuwa na binti wawili, wote wa mama mmoja. Walipokuwa vijana tu, wakiwa wanakaa kule Misri, wakakubali matiti yao kutomaswa, wakapoteza ubikira wao, wakawa malaya. Yule mkubwa aliitwa Ohola, na yule mdogo Oholiba. Basi, wote wakawa wangu, wakanizalia watoto, wa kiume na wa kike. Basi, Ohola ni Samaria na Oholiba ni Yerusalemu! “Ingawa Ohola alikuwa mke wangu, lakini aliendelea kuwa mzinzi na kuwatamani wapenzi wake wa Ashuru. Hao walikuwa askari, wamevalia sare za rangi ya zambarau, watawala na makamanda. Wote walikuwa vijana wa kuvutia na wapandafarasi hodari. Ohola alifanya zinaa na hao maofisa wote wa vyeo vya juu wa Ashuru naye akajitia unajisi kwa vinyago vyote vya kila mwanamume wake aliyemtamani. Aliendelea na uzinzi wake aliouanza kule Misri wakati huo, akiwa bado kijana, wanaume walivunja ubikira wake na kuzitimiza tamaa zao kwake. Kwa hiyo nilimtia mikononi mwa Waashuru wapenzi wake, ambao aliwatamani sana. Hao walimvua mavazi yake na kumwacha uchi. Waliwakamata watoto wake, naye mwenyewe wakamuua kwa upanga. Adhabu hiyo aliyopata ikawa fundisho kwa wanawake wengine. “Oholiba dada yake, aliona jambo hilo, lakini akawa amepotoka kuliko yeye katika tamaa yake na uzinzi wake uliokuwa mbaya kuliko wa dada yake. Aliwatamani sana Waashuru: Wakuu wa mikoa, makamanda, wanajeshi waliovaa sare zao za kijeshi, wapandafarasi hodari, wote wakiwa vijana wa kuvutia. Nilimtambua kuwa najisi. Ama kweli wote wawili walikuwa na tabia hiyo moja. Lakini Oholiba alizidisha uzinzi wake; akapendezwa na picha za Wakaldayo zilizochorwa ukutani, zimetiwa rangi nyekundu, mikanda viunoni, vilemba vikubwa vichwani; hizo zote zilifanana na maofisa, naam, picha ya Wababuloni, wakazi wa nchi ya Wakaldayo. Alipoziona picha hizo, mara akashikwa na tamaa, akatuma wajumbe kwenda Ukaldayo. Basi, Wababuloni wakaja kulala naye. Wakamtia najisi kwa tamaa zao. Alipokwisha tiwa najisi, akajitenga nao. Alipoendelea na uzinzi wake na kufunua uchi wake, mimi nilimwacha kama nilivyomwacha dada yake. Hata hivyo, akazidisha uzinzi wake akifanya kama wakati wa ujana wake alipofanya uzinzi kule Misri. Aliwatamani sana wanaume wenye tamaa mbaya kama ya punda na nguvu nyingi za uzazi kama farasi dume.” “Oholiba aliutamani uchafu wake wa ujana alipokuwa Misri, ambako Wamisri walivunja ubikira wake, na kuyatomasa matiti yake machanga.