Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 35:1-15

Mwanzo 35:1-15 NENO

Kisha Mungu akamwambia Yakobo, “Panda uende Betheli ukakae huko. Ukamjengee Mungu madhabahu huko, Yeye aliyekutokea ulipokuwa unamkimbia Esau ndugu yako.” Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni mliyo nayo, mjitakase na mkabadilishe nguo zenu. Kisha njooni, twende Betheli, mahali nitakapomjengea Mungu madhabahu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, ambaye amekuwa pamoja nami popote nilipoenda.” Kwa hiyo wakampa Yakobo miungu yote ya kigeni waliyokuwa nayo, pamoja na pete zilizokuwa masikioni mwao. Yakobo akavizika chini ya mwaloni ulio Shekemu. Kisha wakaondoka, na utisho wa Mungu ukaipata miji yote iliyowazunguka. Kwa hiyo hakuna aliyewafuatia wana wa Yakobo. Yakobo na watu wote waliokuwa pamoja naye wakafika Luzu (ndio Betheli), katika nchi ya Kanaani. Huko akajenga madhabahu na akapaita mahali pale El-Betheli, kwa sababu mahali pale ndipo Mungu alijifunua kwake alipokuwa akimkimbia ndugu yake. Wakati huu Debora, mlezi wa Rebeka, akafa na akazikwa chini ya mwaloni ulio nje ya Betheli. Kwa hiyo pakaitwa Alon-Bakuthi. Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-Aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki. Mungu akamwambia, “Jina lako ni Yakobo. Lakini hutaitwa tena Yakobo; jina lako litakuwa Israeli.” Kwa hiyo akamwita Israeli. Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi; ukazae na kuongezeka. Taifa na jamii ya mataifa itatoka kwako, nao wafalme watatoka viunoni mwako. Nchi niliyowapa Ibrahimu na Isaka nakupa wewe pia, nami nitawapa wazao wako baada yako.” Kisha Mungu akapanda juu kutoka kwake mahali pale alipozungumza naye. Yakobo akasimamisha nguzo ya jiwe mahali pale Mungu alipozungumza naye, akamimina sadaka ya kinywaji juu yake, pia akamimina mafuta juu yake. Yakobo akapaita mahali pale Mungu alipozungumza naye Betheli.