Hosea 2:2-13
Hosea 2:2-13 NENO
“Mkemeeni mama yenu, mkemeeni, kwa maana yeye si mke wangu, nami si mume wake. Aondoe sura ya uzinzi katika uso wake na uzinzi kati ya matiti yake. Kama sivyo nitamvua nguo zake awe uchi na kumwacha uchi kama siku ile aliyozaliwa. Nitamfanya kama jangwa, nitamgeuza awe nchi ya kiu, nami nitamuua kwa kiu. Sitaonesha upendo wangu kwa watoto wake, kwa sababu ni watoto wa uzinzi. Mama yao amekosa uaminifu na amewachukua mimba katika aibu. Gomeri alisema, ‘Nitawaendea wapenzi wangu, ambao hunipa chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na kinywaji changu.’ Kwa hiyo mimi Mungu nitaizuia njia yake kwa vichaka vya miiba, nitamjengea ukuta ili asiweze kutoka. Gomeri atawafuatia wapenzi wake lakini hatawapata; atawatafuta lakini hatawapata. Kisha atasema, ‘Nitarudi kwa mume wangu kama kwanza, kwa maana nilikuwa na hali njema kuliko sasa.’ Gomeri hajakubali kuwa mimi ndiye niliyempa nafaka, divai mpya na mafuta, niliyemwongezea fedha na dhahabu waliyoitumia kwa kumtumikia Baali. “Kwa hiyo nitachukua nafaka yangu wakati itakapokomaa na divai yangu mpya wakati itakapokuwa tayari. Nitamnyang’anya sufu yangu na kitani yangu iliyokusudiwa kufunika uchi wake. Basi sasa nitaufunua ufisadi wake mbele ya wapenzi wake; hakuna yeyote atakayemtoa mikononi mwangu. Nitakomesha furaha na macheko yake yote: sikukuu zake za mwaka, sikukuu za Miandamo ya Mwezi, siku zake za Sabato, sikukuu zake zote zilizoamriwa. Nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake, ambayo alisema yalikuwa malipo yake kutoka kwa wapenzi wake; nitaifanya kuwa kichaka, nao wanyama pori wataila. Nitamwadhibu kwa ajili ya siku alizowafukizia uvumba Mabaali; alipojipamba kwa pete na kwa vito vya thamani, na kuwaendea wapenzi wake, lakini mimi alinisahau,” asema Mwenyezi Mungu.