Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 21

21
Wabenyamini watafutiwa wake
1Wanaume wa Israeli walikuwa wameapa kiapo kule Mispa, wakasema: “Hapana mtu yeyote wetu atakayemwoza binti yake kwa Mbenyamini.”
2Watu wakaenda Betheli, wakaketi mbele za Mungu hadi jioni, wakapaza sauti zao wakilia kwa uchungu. 3Wakasema, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa nini jambo hili limewapata Waisraeli? Kwa nini kabila moja la Israeli limekosekana?”
4Kesho yake asubuhi na mapema watu wakajenga madhabahu na kuleta sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.
5Ndipo Waisraeli wakauliza, “Ni kabila lipi la Israeli ambalo halikukusanyika mbele za Mwenyezi Mungu?” Kwa kuwa walikuwa wameapa kiapo kikuu kuwa yeyote asiyefika mbele za Mwenyezi Mungu huko Mispa, kwa hakika angeuawa.
6Basi Waisraeli wakahuzunika kwa ajili ya ndugu zao Wabenyamini, wakasema, “Leo kabila moja limekatiliwa mbali na Israeli. 7Sasa tutawezaje kuwapa binti zetu kuwa wake zao, hao waliobaki, na tumeapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hatutawapa binti zetu kuwa wake zao?” 8Ndipo wakasema, “Ni kabila lipi la Israeli ambalo halikukusanyika mbele za Mwenyezi Mungu huko Mispa?” Wakagundua kuwa hakuna hata mmoja kutoka Yabesh-Gileadi aliyefika kambini kwa kusanyiko. 9Kwa kuwa walipohesabu waliona hapakuwa mtu yeyote wa Yabesh-Gileadi.
10Ndipo mkutano wakatuma wapiganaji elfu kumi na mbili, wakawaamuru kwenda Yabesh-Gileadi na kuua kwa panga wale wote walioishi huko, wakiwemo wake na watoto. 11Wakasema, “Hili ndilo mtakalofanya: Ueni kila mwanaume na kila mwanamke ambaye si bikira.” 12Wakapata kati ya watu walioishi Yabesh-Gileadi wanawali mia nne, mabikira, nao wakawachukua kwenye kambi huko Shilo katika nchi ya Kanaani.
13Ndipo mkutano ukatuma ujumbe wa amani kwa Wabenyamini huko katika mwamba wa Rimoni. 14Basi Wabenyamini wakarudi wakati ule, nao wakapewa wale wanawali wa Yabesh-Gileadi waliohifadhiwa. Lakini hawakuwatosha wanaume wote.
15Waisraeli wakahuzunika kwa ajili ya Wabenyamini, kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa ameweka ufa katika makabila ya Israeli. 16Viongozi wa kusanyiko wakasema, “Kwa kuwa wanawake wa Wabenyamini wameangamizwa, tufanyeje ili kuwapatia wake wale wanaume waliosalia?” 17Wakaendelea kusema, “Lazima tuwape Wabenyamini waliopona wake ili wawe na warithi, nalo kabila lolote katika Israeli lisifutike. 18Hatuwezi kuwapa binti zetu kuwa wake, kwa kuwa sisi Waisraeli tumeapa kiapo hiki: ‘Alaaniwe mtu yeyote ampaye Mbenyamini mke.’ ” 19Ndipo waliposema, “Tazama iko sikukuu ya kila mwaka ya Mwenyezi Mungu katika Shilo, kaskazini mwa Betheli na mashariki mwa ile barabara inayotoka Betheli kwenda Shekemu, upande wa kusini wa Lebona.”
20Hivyo wakawaelekeza Wabenyamini, wakisema, “Nendeni mkajifiche kwenye mashamba ya mizabibu, 21na mkae macho. Wasichana wa Shilo watakapojiunga kwenye kucheza, tokeni kwenye hayo mashamba ya mizabibu, na kila mmoja ajinyakulie mke kutoka miongoni mwa hao wasichana wa Shilo, nanyi mwende nao katika nchi ya Benyamini. 22Baba zao au ndugu zao watakapotulalamikia, tutawaambia, ‘Kuweni wakarimu kwetu, nanyi mturuhusu tuwe nao kwa kuwa hatukuweza kumpa kila mtu mke tulipopigana. Lakini ninyi pia hamna hatia, kwa kuwa hamkuwapa wao binti zenu kuwa wake.’ ”
23Basi hivyo ndivyo Wabenyamini walivyofanya. Wasichana walipokuwa wakicheza, kila mtu akanyakua msichana mmoja, akaenda naye ili awe mke wake. Kisha wakarudi katika urithi wao na kuijenga upya miji na kuishi humo.
24Wakati huo Waisraeli wakaondoka sehemu ile na kwenda nyumbani kwao, kwa makabila yao na kwa jamaa zao, kila mmoja kwenye urithi wake mwenyewe.
25Katika siku hizo, Waisraeli hawakuwa na mfalme; kila mtu alifanya alivyoona ni vyema machoni pake.

Iliyochaguliwa sasa

Waamuzi 21: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia