Yohana 18:15-27
Yohana 18:15-27 NEN
Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walikuwa wakimfuata Yesu. Huyu mwanafunzi mwingine alikuwa anafahamika kwa kuhani mkuu, hivyo aliingia ndani ya ukumbi pamoja na Yesu. Lakini Petro alisimama nje karibu na lango, ndipo yule mwanafunzi mwingine, aliyejulikana na kuhani mkuu, akazungumza na msichana aliyekuwa analinda lango, akamruhusu Petro aingie ndani. Yule msichana akamuuliza Petro, “Je, wewe pia si mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?” Petro akajibu, “Sio mimi.” Wale watumishi na askari walikuwa wamesimama wakiota moto wa makaa kwa sababu palikuwa na baridi, Petro naye alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto. Wakati huo kuhani mkuu akawa anamuuliza Yesu kuhusu wanafunzi wake na mafundisho yake. Yesu akamjibu, “Nimekuwa nikizungumza waziwazi mbele ya watu wote. Siku zote nimefundisha katika masinagogi na Hekaluni, mahali ambapo Wayahudi wote hukusanyika. Sikusema jambo lolote kwa siri. Mbona unaniuliza mimi maswali? Waulize wale walionisikia yale niliyowaambia. Wao wanajua niliyosema.” Alipomaliza kusema hayo, mmoja wa askari aliyekuwa amesimama karibu naye, akampiga Yesu kofi usoni, kisha akasema, “Je, hivyo ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?” Yesu akamjibu akasema, “Kama nimesema jambo baya, shuhudia huo ubaya niliousema. Lakini kama nimesema yaliyo kweli, mbona umenipiga?” Ndipo Anasi akampeleka Yesu kwa kuhani mkuu Kayafa, akiwa bado amefungwa. Wakati huo Simoni Petro alikuwa amesimama akiota moto. Baadhi ya wale waliokuwepo wakamuuliza, “Je, wewe si mmoja wa wanafunzi wake?” Petro akakana, akasema, “Sio mimi.” Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu, ndugu yake yule mtu ambaye Petro alikuwa amemkata sikio, akamuuliza, “Je, mimi sikukuona kule bustanini ukiwa na Yesu?” Kwa mara nyingine tena Petro akakana, naye jogoo akawika wakati huo huo.