Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 18:15-27

Yohane 18:15-27 BHN

Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata Yesu. Huyo mwanafunzi mwingine alikuwa anajulikana kwa kuhani mkuu, hivyo aliingia pamoja na Yesu ndani ya ukumbi wa kuhani mkuu. Lakini Petro alikuwa amesimama nje, karibu na mlango. Basi, huyo mwanafunzi mwingine aliyekuwa anajulikana kwa kuhani mkuu alitoka nje akasema na mjakazi, mngojamlango, akamwingiza Petro ndani. Huyo mjakazi mngojamlango akamwuliza Petro, “Je, nawe pia ni mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?” Petro akamwambia, “Si mimi!” Watumishi na walinzi walikuwa wamewasha moto kwa sababu kulikuwa na baridi, wakawa wanaota moto. Naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto. Basi, kuhani mkuu akamwuliza Yesu juu ya wanafunzi wake na mafundisho yake. Yesu akamjibu, “Nimesema na kila mtu daima hadharani. Kila mara nimefundisha katika masunagogi na hekaluni, mahali wanapokutana Wayahudi wote; na wala sijasema chochote kwa siri. Kwa nini waniuliza mimi? Waulize wale waliosikia nini niliwaambia. Wao wanajua niliyowaambia.” Alipokwisha sema hayo mlinzi mmoja aliyekuwa amesimama hapo akampiga kofi akisema, “Je, ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?” Yesu akamjibu, “Kama nimesema vibaya, onesha huo ubaya; lakini ikiwa nimesema vema, mbona wanipiga?” Basi, Anasi akampeleka Yesu akiwa amefungwa, kwa kuhani mkuu Kayafa. Petro alikuwa hapo akiota moto. Basi, wakamwuliza, “Je, nawe pia si mmoja wa wanafunzi wake?” Yeye akakana na kusema, “Si mimi!” Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu, jamaa wa yule aliyekatwa sikio na Petro, akamwuliza, “Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?” Petro akakana tena; mara jogoo akawika.