Yohana 7:37-52
Yohana 7:37-52 NENO
Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Isa akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe. Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yanavyosema, vijito vya maji ya uzima vitatiririka kutoka ndani yake.” Isa aliposema haya, alimaanisha Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye wote waliomwamini wangempokea. Kwa maana hadi wakati huo Roho wa Mungu alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Isa alikuwa bado hajatukuzwa. Waliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa umati ule wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.” Wengine wakasema, “Huyu ndiye Al-Masihi!” Lakini wengine wakauliza, “Je, Al-Masihi kwao ni Galilaya? Je, Maandiko hayasemi kwamba Al-Masihi atakuja kutoka jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?” Kwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Isa. Baadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa. Hatimaye wale walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliokuwa wamewatuma ili kumkamata Isa, wakaulizwa, “Mbona hamkumkamata?” Wale walinzi wakajibu, “Kamwe hajanena mtu yeyote kama yeye anenavyo.” Mafarisayo wakajibu, “Je, nanyi pia mmedanganyika? Je, kuna kiongozi yeyote au mmoja wa Mafarisayo ambaye amemwamini? Lakini umati huu wa watu wasiojua Torati ya Musa, wamelaaniwa.” Ndipo Nikodemo, yule aliyekuwa amemwendea Isa siku moja usiku, na alikuwa mmoja wao, akauliza, “Je, sheria zetu zinaturuhusu kumhukumu mtu kabla ya kumsikiliza na kufahamu alilotenda?” Wakamjibu, “Je, wewe pia unatoka Galilaya? Chunguza nawe utaona kwamba hakuna nabii atokae Galilaya!” [