Yn 7:37-52
Yn 7:37-52 SUV
Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa. Basi wengine katika mkutano walipoyasikia maneno hayo, walisema, Hakika huyu ndiye nabii yule. Wengine walisema, Huyu ndiye Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya? Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi? Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika. Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, Mbona hamkumleta? Wale watumishi wakajibu. Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena. Basi Mafarisayo wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika? Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo? Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa. Akawaambia Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao), Je! Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo? Wakajibu, wakamwambia, Je! Wewe nawe umetoka Galilaya! Tafuta, ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.