Ayubu 30:16-31
Ayubu 30:16-31 NENO
“Sasa maisha yangu yamefikia mwisho; siku za mateso zimenikamata. Usiku mifupa yangu inachoma; maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe. Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo; hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu. Yeye amenitupa kwenye matope, nami nimekuwa kama mavumbi na majivu. “Ee Mwenyezi Mungu, ninakulilia wewe lakini hunijibu; ninasimama, nawe unanitazama tu. Wewe unanigeukia bila huruma; unanishambulia kwa nguvu za mkono wako. Unaninyakua na kunipeperusha kwa upepo; umenirusharusha kwenye dhoruba. Ninajua utanileta hadi kifoni, mahali wenye uhai wote wamewekewa. “Hakika hakuna mtu anayemshambulia mhitaji anapoomba msaada katika shida yake. Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu? Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini? Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia; nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja. Kusukwasukwa ndani yangu kamwe hakutulii; siku za mateso zinanikabili. Ninazunguka nikiwa nimeungua, lakini si kwa jua; ninasimama katika kusanyiko nikiomba msaada. Nimekuwa ndugu wa mbweha, rafiki wa mabundi. Ngozi yangu imekuwa nyeusi nayo inachunika; mifupa yangu inaungua kwa homa. Kinubi changu kimegeuka kuwa maombolezo, nayo filimbi yangu imekuwa sauti ya kilio.