Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 1:1-11

Maombolezo 1:1-11 NEN

Tazama jinsi mji ulivyoachwa ukiwa, mji ambao zamani ulikuwa umejaa watu! Jinsi ambavyo umekuwa kama mama mjane, ambaye wakati fulani alikuwa maarufu miongoni mwa mataifa! Yule ambaye alikuwa malkia miongoni mwa majimbo sasa amekuwa mtumwa. Kwa uchungu, hulia sana usiku, machozi yapo kwenye mashavu yake. Miongoni mwa wapenzi wake wote hakuna yeyote wa kumfariji. Rafiki zake wote wamemsaliti, wamekuwa adui zake. Baada ya mateso na kufanyishwa kazi kikatili, Yuda amekwenda uhamishoni. Anakaa miongoni mwa mataifa, hapati mahali pa kupumzika. Wote ambao wanamsaka wamemkamata katikati ya dhiki yake. Barabara zielekeazo Sayuni zaomboleza, kwa kuwa hakuna yeyote anayekuja kwenye sikukuu zake zilizoamriwa. Malango yake yote yamekuwa ukiwa, makuhani wake wanalia kwa uchungu, wanawali wake wanahuzunika, naye yuko katika uchungu wa maumivu makuu. Adui zake wamekuwa mabwana zake, watesi wake wana raha. BWANA amemletea huzuni kwa sababu ya dhambi zake nyingi. Watoto wake wamekwenda uhamishoni, mateka mbele ya adui. Fahari yote imeondoka kutoka kwa Binti Sayuni. Wakuu wake wako kama ayala ambaye hapati malisho, katika udhaifu wamekimbia mbele ya anayewasaka. Katika siku za mateso yake na kutangatanga, Yerusalemu hukumbuka hazina zote ambazo zilikuwa zake siku za kale. Wakati watu wake walipoanguka katika mikono ya adui, hapakuwepo na yeyote wa kumsaidia. Watesi wake walimtazama na kumcheka katika maangamizi yake. Yerusalemu ametenda dhambi sana kwa hiyo amekuwa najisi. Wote waliomheshimu wanamdharau, kwa maana wameuona uchi wake. Yeye mwenyewe anapiga kite na kugeukia mbali. Uchafu wake umegandamana na nguo zake; hakuwaza juu ya maisha yake ya baadaye. Anguko lake lilikuwa la kushangaza, hapakuwepo na yeyote wa kumfariji. “Tazama, Ee BWANA, teso langu, kwa maana adui ameshinda.” Adui ametia mikono juu ya hazina zake zote, aliona mataifa ya kipagani wakiingia mahali patakatifu pake, wale uliowakataza kuingia kwenye kusanyiko lako. Watu wake wote wanalia kwa uchungu watafutapo chakula; wanabadilisha hazina zao kwa chakula ili waweze kuendelea kuishi. “Tazama, Ee BWANA, ufikiri, kwa maana nimedharauliwa.”