Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Omb 1:1-11

Omb 1:1-11 SUV

Jinsi mji huu ukaavyo ukiwa, Huo uliokuwa umejaa watu! Jinsi alivyokuwa kama mjane, Yeye aliyekuwa mkuu kati ya mataifa! Binti mfalme kati ya majimbo, Jinsi alivyoshikwa shokoa! Hulia sana wakati wa usiku, Na machozi yake yapo mashavuni; Miongoni mwa wote waliompenda Hakuna hata mmoja amfarijiye; Rafiki zake wote wamemtenda hila, Wamekuwa adui zake. Yuda amehamishwa kwa sababu ya kuonewa, Na kwa sababu ya utumwa mkuu; Anakaa kati ya makafiri, Haoni raha iwayo yote; Wote waliomfuata wamempata Katika dhiki yake. Njia za Sayuni zaomboleza, Kwa kuwa hakuna ajaye kwa sikukuu; Malango yake yote yamekuwa ukiwa, Makuhani wake hupiga kite; Wanawali wake wanahuzunika; Na yeye mwenyewe huona uchungu. Watesi wake wamekuwa kichwa, Adui zake hufanikiwa; Kwa kuwa BWANA amemtesa Kwa sababu ya wingi wa makosa yake; Watoto wake wadogo wamechukuliwa mateka Mbele yake huyo mtesi. Naye huyo binti Sayuni Enzi yake yote imemwacha; Wakuu wake wamekuwa kama ayala Wasioona malisho; Nao wamekwenda zao hawana nguvu Mbele yake anayewafuatia. Siku za mateso na misiba yake, Yerusalemu huyakumbuka matamaniko yake yote Yaliyokuwa tangu siku za kale; Hapo watu wake walipoanguka mikononi mwa mtesi, Wala hakuna hata mmoja wa kumsaidia; Hao watesi wake walimwona, Wakafanya sabato zake kuwa mzaha. Yerusalemu amefanya dhambi sana; Kwa hiyo amekuwa kama kitu kichafu; Wote waliomheshimu wanamdharau, Kwa sababu wameuona uchi wake; Naam, yeye anaugua, Na kujigeuza aende nyuma. Uchafu wake ulikuwa katika marinda yake; Hakukumbuka mwisho wake; Kwa hiyo ameshuka kwa ajabu; Yeye hana mtu wa kumfariji; Tazama, BWANA, teso langu; Maana huyo adui amejitukuza. Huyo mtesi amenyosha mkono wake Juu ya matamaniko yake yote; Maana ameona ya kuwa makafiri wameingia Ndani ya patakatifu pake; Ambao kwa habari zao wewe uliamuru Wasiingie katika kusanyiko lako. Watu wake wote hupiga kite, Wanatafuta chakula; Wameyatoa matamaniko yao wapate chakula Cha kuihuisha nafsi; Ee BWANA, tazama, uangalie; Kwa maana mimi nimekuwa mnyonge.