Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 13:14-27

Marko 13:14-27 NEN

“Mtakapoona ‘chukizo la uharibifu’ limesimama mahali pasipolipasa (asomaye na afahamu), basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani. Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke au kuingia ndani ili kuchukua chochote. Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Ombeni mambo haya yasitokee wakati wa baridi. Kwa maana siku hizo zitakuwa za dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo, hapo Mungu alipoumba ulimwengu, mpaka leo, na wala haitakuwako tena kamwe. Kama Bwana asingelifupisha siku hizo, kamwe asingeliokoka mtu yeyote. Lakini kwa ajili ya wateule, wale aliowachagua, amezifupisha siku hizo. Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ au, ‘Tazama, yuko kule,’ msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara na maajabu ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule. Hivyo jihadharini. Nimekwisha kuwaambia mambo haya yote mapema kabla hayajatukia. “Lakini katika siku hizo, baada ya hiyo dhiki, “ ‘jua litatiwa giza nao mwezi hautatoa nuru yake; nazo nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za anga zitatikisika.’ “Ndipo watu wote watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. Naye atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka miisho ya dunia hadi miisho ya mbingu.