Marko 13:14-27
Marko 13:14-27 BHN
“Mtakapoona ‘Chukizo Haribifu limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake), hapo, walioko Yudea wakimbilie milimani. Aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu. Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi. Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena. Kama Bwana asingepunguza siku hizo hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo. “Basi mtu akiwaambieni, ‘Tazama, Kristo yupo hapa,’ au ‘Yupo pale,’ msimsadiki. Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, kwa ajili ya kuwapotosha wateule wa Mungu kama ikiwezekana. Lakini nyinyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea. “Basi, siku hizo, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza. Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu. Kisha atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.