Marko 13:14-27
Marko 13:14-27 SRUV
Lakini mlionapo chukizo la uharibifu likisimama pasipolipasa, (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Yudea na wakimbilie milimani; na mtu aliye juu ya dari asishuke, wala asiingie kuchukua kitu nyumbani mwake; naye aliye shambani asirudi nyuma kulichukua vazi lake. Lakini ole wao wenye mimba, nao wanyonyeshao siku hizo! Ila ombeni yasitokee hayo wakati wa baridi. Kwa maana siku hizo zitakuwa na dhiki, jinsi isivyokuwa tangu mwanzo wa kuumba alipoumba Mungu hata sasa, wala haitakuwa kamwe. Na kama Bwana asingalizikatiza siku hizo, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule aliowateua amezikatiza siku hizo. Na wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule, msisadiki; kwa maana watajitokeza Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, ikiwezekana, hata hao wateule. Bali ninyi jihadharini; nimekwisha kuwaonya yote mbele. Lakini siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hatautoa mwanga wake. Na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu.