Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 15:1-20

Marko 15:1-20 NEN

Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani, pamoja na wazee, walimu wa sheria na Baraza lote, wakafikia uamuzi. Wakamfunga Yesu, wakamchukua na kumkabidhi kwa Pilato. Pilato akamuuliza, “Je, wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Wewe umesema.” Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi. Pilato akamuuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.” Lakini Yesu hakujibu lolote, hivyo Pilato akashangaa. Ilikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa yeyote ambaye watu wangemtaka. Wakati huo, mtu aliyeitwa Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wametekeleza uuaji wakati wa maasi. Ule umati wa watu ukamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake. Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu Mfalme wa Wayahudi?” Kwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Yesu mikononi mwake kwa ajili ya wivu. Lakini viongozi wa makuhani wakauchochea ule umati wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake. Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?” Wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe!” Pilato akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?” Lakini wao wakapiga kelele kwa nguvu zaidi, wakisema, “Msulubishe!” Pilato, akitaka kuuridhisha ule umati wa watu, akawafungulia Baraba. Naye baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe. Askari wakampeleka Yesu hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio, wakakusanya kikosi kizima cha askari. Wakamvalisha Yesu joho la zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani. Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake, wakamsujudia kwa kumdhihaki. Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulubishe.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Marko 15:1-20