Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 15:1-20

Marko 15:1-20 SRUV

Mara kulipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani walifanya shauri pamoja na wazee na waandishi na baraza nzima, wakamfunga Yesu, wakamchukua, wakamleta mbele ya Pilato. Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu, akamwambia, Wewe wasema. Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi. Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki! Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu. Basi wakati wa sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, wamwombaye. Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, aliyefungwa pamoja na waasi, waliosababisha mauaji katika uhalifu huo. Makutano wakaja, wakaanza kuomba awafanyie kama vile alivyozoea. Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi? Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa husuda. Lakini wakuu wa makuhani wakawachochea watu, kuwa afadhali awafungulie Baraba. Pilato akajibu tena akawaambia, Basi nimtendeje huyu mnayemnena kuwa ni mfalme wa Wayahudi? Wakapiga kelele tena, Msulubishe. Pilato akawaambia, Kwani ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulubishe. Pilato kwa kupenda kuwaridhisha watu, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulubiwe. Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, makao makuu ya mtawala), wakakusanya pamoja kikosi kizima. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji la miiba, wakamtia kichwani; wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia. Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakampeleka nje ili wamsulubishe.

Soma Marko 15

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Marko 15:1-20