Mithali 13:1-25
Mithali 13:1-25 NEN
Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya babaye, bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. Kutoka tunda la midomo yake mtu hufurahia mambo mema, bali wasio waaminifu wanatamani sana jeuri. Yeye alindaye midomo yake hulinda nafsi yake, bali yeye asemaye kwa haraka ataangamia. Mvivu hutamani sana na hapati kitu, bali nafsi ya mwenye bidii hutoshelezwa kikamilifu. Mwenye haki huchukia uongo, bali waovu huleta aibu na fedheha. Haki humlinda mtu mwadilifu, bali uovu humwangusha mwenye dhambi. Mtu mmoja hujifanya tajiri, kumbe hana chochote; mwingine hujifanya maskini, kumbe ana utajiri mwingi. Utajiri wa mtu waweza kukomboa maisha yake, bali mtu maskini hasikii kitisho. Nuru ya mwenye haki hungʼaa sana, bali taa ya mwovu itazimwa. Kiburi huzalisha magomvi tu, bali hekima hupatikana kwa wale wanaozingatia ushauri. Fedha isiyo ya halali hupungua, bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka. Kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua, bali tumaini lililotimizwa ni mti wa uzima. Yeye anayedharau mafundisho anajiletea maangamizi, bali yeye anayeheshimu agizo hupewa tuzo. Mafundisho ya mwenye busara ni chemchemi ya uzima, ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti. Ufahamu mzuri hupata upendeleo, bali njia ya asiye mwaminifu ni ngumu. Kila mwenye busara hutenda kwa maarifa, bali mpumbavu hudhihirisha upumbavu wake. Mjumbe mwovu huanguka kwenye taabu, bali mjumbe mwaminifu huleta uponyaji. Yeye anayedharau maonyo hupata umaskini na aibu, bali yeye anayekubali maonyo huheshimiwa. Tarajio lililotimizwa ni tamu kwa nafsi, bali wapumbavu huchukia sana kuacha ubaya. Yeye atembeaye na mwenye hekima atapata hekima, bali rafiki wa mpumbavu hupata madhara. Balaa humwandama mtenda dhambi, bali mafanikio ni thawabu kwa mwenye haki. Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi, bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa kwa ajili ya wenye haki. Shamba la mtu maskini laweza kuzalisha chakula kingi, bali dhuluma hukifutilia mbali. Yeye aizuiaye fimbo yake hampendi mwanawe, bali yeye ampendaye huwa mwangalifu kumwadibisha. Mwenye haki hula mpaka akaridhisha moyo wake, bali tumbo la mwovu hutaabika kwa njaa.