Mit 13:1-25
Mit 13:1-25 SUV
Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri. Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu. Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu. Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi. Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu; Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi. Dia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lo lote. Nuru ya mwenye haki yang’aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika. Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana. Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa. Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima. Kila alidharauye neno hujiletea uharibifu; Bali yeye aiogopaye amri atapewa thawabu. Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti. Ufahamu mwema huleta upendeleo; Bali njia ya haini huparuza. Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali mpumbavu hueneza upumbavu. Mjumbe mbaya huanguka maovuni; Bali mjumbe mwaminifu ni afya. Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa; Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa. Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu; Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu. Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. Uovu huwaandamia wenye dhambi; Bali mwenye haki atalipwa mema. Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki. Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini; Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma. Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema. Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa.