Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 8:1-21

Mithali 8:1-21 NEN

Je, hekima haitani? Je, ufahamu hapazi sauti? Juu ya miinuko karibu na njia, penye njia panda, ndipo asimamapo; kando ya malango yaelekeayo mjini, kwenye maingilio, hulia kwa sauti kubwa, akisema: “Ni ninyi wanaume, ninaowaita; ninapaza sauti yangu kwa wanadamu wote. Ninyi ambao ni wajinga, pateni akili; ninyi mlio wapumbavu, pateni ufahamu. Sikilizeni, kwa maana nina mambo muhimu ya kusema; ninafungua midomo yangu kusema lililo sawa. Kinywa changu husema lililo kweli, kwa maana midomo yangu huchukia uovu. Maneno yote ya kinywa changu ni haki; hakuna mojawapo lililopotoka wala ukaidi. Kwa wenye kupambanua yote ni sahihi; hayana kasoro kwa wale wenye maarifa. Chagua mafundisho yangu badala ya fedha, maarifa badala ya dhahabu safi, kwa maana hekima ina thamani kuliko marijani na hakuna chochote unachohitaji kinacholingana naye. “Mimi hekima, nakaa pamoja na busara; ninamiliki maarifa na busara. Kumcha BWANA ni kuchukia uovu; ninachukia kiburi na majivuno, tabia mbaya na mazungumzo potovu. Ushauri na hukumu sahihi ni vyangu; nina ufahamu na nina nguvu. Kwa msaada wangu wafalme hutawala na watawala hutunga sheria zilizo za haki, kwa msaada wangu wakuu hutawala, na wenye vyeo wote watawalao dunia. Nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona. Utajiri na heshima viko kwangu, utajiri udumuo na mafanikio. Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi; kile nitoacho hupita fedha iliyo bora. Natembea katika njia ya unyofu katika mapito ya haki, nawapa utajiri wale wanipendao na kuzijaza hazina zao.