Zaburi 145
145
Zaburi 145#145:0 Zaburi hii imetungwa kila mstari (ikiwa ni pamoja na 13b) ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
Wimbo wa kusifu ukuu na wema wa Mwenyezi Mungu
Wimbo wa sifa. Wa Daudi.
1Nitakutukuza wewe, Mungu wangu Mfalme,
nitalisifu jina lako milele na milele.
2Kila siku nitakusifu
na kulitukuza jina lako milele na milele.
3Mwenyezi Mungu ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,
ukuu wake haupimiki.
4Kizazi kimoja kitasifia kazi zako kwa kizazi kingine,
watasimulia matendo yako makuu.
5Watasema juu ya utukufu wa fahari ya ukuu wako,
nami nitatafakari juu ya kazi zako za ajabu.
6Watasimulia uwezo wa kazi zako za kutisha,
nami nitatangaza matendo yako makuu.
7Wataadhimisha wema wako mwingi,
na wataimba kwa shangwe kuhusu haki yako.
8Mwenyezi Mungu ni mwenye neema na mwingi wa huruma,
si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo.
9Mwenyezi Mungu ni mwema kwa wote,
ana huruma kwa vyote alivyovifanya.
10Ee Mwenyezi Mungu, vyote ulivyovifanya vitakusifu,
watakatifu wako watakutukuza.
11Watasimulia utukufu wa ufalme wako
na kusema kuhusu ukuu wako,
12ili watu wote wajue matendo yako makuu
na utukufu wa fahari ya ufalme wako.
13Ufalme wako ni ufalme wa milele,
mamlaka yako hudumu vizazi vyote.
Mwenyezi Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake zote
na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.
14Mwenyezi Mungu huwategemeza wote waangukao,
na huwainua wote waliolemewa na mizigo yao.
15Macho ya watu wote yanakutazama,
nawe huwapa chakula chao wakati wake.
16Waufumbua mkono wako,
watosheleza haja ya kila kitu kilicho hai.
17Mwenyezi Mungu ni mwenye haki katika njia zake zote,
na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.
18Mwenyezi Mungu yu karibu na wote wamwitao,
karibu na wote wamwitao kwa uaminifu.
19Huwatimizia wamchao matakwa yao,
husikia kilio chao na kuwaokoa.
20Mwenyezi Mungu huwalinda wote wanaompenda,
bali waovu wote atawaangamiza.
21Kinywa changu kitazinena sifa za Mwenyezi Mungu.
Kila kiumbe na kilisifu jina lake takatifu
milele na milele.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 145: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.