Zaburi 49:1-12
Zaburi 49:1-12 NEN
Sikieni haya, enyi mataifa yote, sikilizeni, ninyi wote mkaao dunia hii. Wakubwa kwa wadogo, matajiri na maskini pamoja: Kinywa changu kitasema maneno ya hekima, usemi wa moyo wangu utatoa ufahamu. Nitatega sikio langu nisikilize mithali, nitafafanua kitendawili kwa zeze: Kwa nini niogope siku mbaya zinapokuja, wakati wadanganyifu waovu wanaponizunguka, wale wanaotegemea mali zao na kujivunia utajiri wao mwingi? Hakuna mwanadamu awaye yote awezaye kuukomboa uhai wa mwingine, au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake. Fidia ya uhai ni gharama kubwa, hakuna malipo yoyote yanayotosha, ili kwamba aishi milele na asione uharibifu. Wote wanaona kwamba watu wenye hekima hufa; wajinga na wapumbavu vivyo hivyo huangamia na kuwaachia wengine mali zao. Makaburi yao yatabaki kuwa nyumba zao za milele, makao yao vizazi vyote; ingawa walikuwa na mashamba na kuyaita kwa majina yao. Lakini mwanadamu, licha ya utajiri wake, hadumu; anafanana na mnyama aangamiaye.