Zaburi 78:56-72
Zaburi 78:56-72 NEN
Lakini wao walimjaribu Mungu, na kuasi dhidi ya Yeye Aliye Juu Sana, wala hawakuzishika sheria zake. Kama baba zao, hawakuwa thabiti wala waaminifu, wakawa wasioweza kutegemewa kama upinde wenye kasoro. Wakamkasirisha Mungu kwa mahali pao pa juu pa kuabudia miungu, wakachochea wivu wake kwa sanamu zao. Wakati Mungu alipowasikia, alikasirika sana, akamkataa Israeli kabisa. Akaiacha hema ya Shilo, hema aliyokuwa ameiweka katikati ya wanadamu. Akalipeleka Sanduku la nguvu zake utumwani, utukufu wake mikononi mwa adui. Aliachia watu wake wauawe kwa upanga, akaukasirikia sana urithi wake. Moto uliwaangamiza vijana wao, na wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi, makuhani wao waliuawa kwa upanga, wala wajane wao hawakuweza kulia. Ndipo Bwana alipoamka kama vile kuamka usingizini, kama vile mtu aamkavyo kutoka kwenye bumbuazi la mvinyo. Aliwapiga na kuwashinda adui zake, akawatia katika aibu ya milele. Ndipo alipozikataa hema za Yosefu, hakulichagua kabila la Efraimu, lakini alilichagua kabila la Yuda, Mlima Sayuni, ambao aliupenda. Alijenga patakatifu pake kama vilele, kama dunia ambayo aliimarisha milele. Akamchagua Daudi mtumishi wake na kumtoa kwenye mazizi ya kondoo. Kutoka kuchunga kondoo alimleta kuwa mchungaji wa watu wake Yakobo, wa Israeli urithi wake. Naye Daudi aliwachunga kwa uadilifu wa moyo, kwa mikono ya ustadi aliwaongoza.