Zaburi 78:56-72
Zaburi 78:56-72 BHN
Hata hivyo walimjaribu na kumwasi Mungu Mkuu; wala hawakuzingatia masharti yake. Ila waligeuka na kufanya mabaya kama wazee wao; wakayumbayumba kama upinde usio imara. Walimkasirisha kwa madhabahu zao za miungu; wakamchochea aone wivu kwa sanamu zao za kuchonga. Mungu alipoona hayo, akawaka hasira; akamkataa Israeli katakata. Aliyaacha makao yake kule Shilo, makao ambamo alikaa kati ya watu. Aliiacha ishara ya nguvu yake itekwe, utukufu wake utiwe mikononi mwa maadui. Aliwakasirikia watu wake mwenyewe; akawatoa waangamizwe kwa upanga. Moto ukawateketeza vijana wao wa kiume, na wasichana wao wakakosa wachumba. Makuhani wao walikufa kwa upanga, wala wajane wao hawakuomboleza. Kisha Bwana aliamka kama kutoka usingizini, kama shujaa aliyechangamshwa na divai. Akawatimua maadui zake; akawatia aibu ya kudumu milele. Lakini aliikataa jamaa ya Yosefu, wala hakulichagua kabila la Efraimu. Ila alilichagua kabila la Yuda, mlima Siyoni anaoupenda. Alijenga hapo hekalu lake kubwa kama mbingu, kama dunia aliyoiweka imara milele. Alimchagua Daudi, mtumishi wake, akamtoa katika kazi ya kuchunga kondoo. Alimtoa katika kazi ya kuchunga kondoo na wanakondoo, awe na jukumu la kuchunga watu wa Yakobo taifa lake. Achunge Israeli, watu wake Mungu mwenyewe. Daudi akawafunza kwa moyo wake wote, akawaongoza kwa uhodari mkubwa.