Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 19:1-10

Ufunuo 19:1-10 NEN

Baada ya haya nikasikia sauti kama ya umati mkubwa mbinguni wakipiga kelele wakisema: “Haleluya! Wokovu na utukufu na uweza ni vya Mungu wetu, kwa maana hukumu zake ni za kweli na za haki. Amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake. Mungu amemlipiza kisasi kwa ajili ya damu ya watumishi wake.” Wakasema tena kwa nguvu: “Haleluya! Moshi wake huyo kahaba unapanda juu milele na milele.” Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wanne wenye uhai wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu: “Amen, Haleluya!” Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema: “Msifuni Mungu wetu, ninyi watumishi wake wote, ninyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa!” Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipiga kelele wakisema: “Haleluya! Kwa maana BWANA Mungu wetu Mwenyezi anatawala. Tufurahi, tushangilie na kumpa utukufu! Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia na bibi arusi wake amejiweka tayari. Akapewa kitani safi, nyeupe inayongʼaa, ili avae.” (Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.) Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.” Ndipo nikaanguka kifudifudi miguuni pake ili kumwabudu, lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.”