Ufunuo 19:1-10
Ufunuo 19:1-10 SRUV
Baada ya hayo nikasikia sauti kama sauti ya mikutano mikubwa, sauti kubwa mbinguni, ikisema, Haleluya; Wokovu na utukufu na nguvu zina Bwana Mungu wetu; kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake. Wakasema mara ya pili, Haleluya. Na moshi wake hupaa juu hata milele na milele. Na wale wazee ishirini na wanne, na wale wenye uhai wanne, wakasujudu na kumwabudu Mungu, aketiye katika kile kiti cha enzi, wakisema, Amina, Haleluya. Sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Msifuni Mungu wetu, enyi watumwa wake wote, ninyi mnaomcha, wadogo kwa wakubwa. Nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, na kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi yenye nguvu, ikisema, Haleluya; kwa kuwa Bwana Mungu wetu, Mwenyezi, amemiliki. Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari. Naye ameruhusiwa kuvikwa kitani nzuri, ing'aayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu. Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa katika karamu ya arusi ya Mwana-kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu. Nami nikaanguka mbele ya miguu yake, ili nimsujudie; akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mtumishi mwenzako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.