Amo 7:1-9
Amo 7:1-9 SUV
Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, aliumba nzige mwanzo wa kuchipuka kwake mimea wakati wa vuli; na tazama, ilikuwa mimea ya wakati wa vuli baada ya mavuno ya mfalme. Ikawa, nzige walipokwisha kula majani ya nchi, ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, samehe, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. BWANA akaghairi katika jambo hili. Jambo hili halitakuwa, asema BWANA. Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, Bwana MUNGU aliita ili kushindana kwa moto; nao ukavila vilindi vikuu, ukataka kuiteketeza nchi kavu. Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, acha, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. BWANA akaghairi katika jambo hili pia. Jambo hili halitakuwa, asema Bwana MUNGU. Haya ndiyo aliyonionyesha; na tazama, Bwana alisimama karibu na ukuta uliojengwa kwa timazi, mwenye timazi mkononi mwake. BWANA akaniambia, Amosi, unaona nini? Nikasema, Naona timazi. Ndipo Bwana akasema, Tazama, nitaweka timazi kati ya watu wangu Israeli; sitawapita tena kamwe; na mahali palipoinuka pa Isaka patakuwa ukiwa, na mahali patakatifu pa Israeli pataharibika; nami nitaondoka nishindane na nyumba ya Yeroboamu kwa upanga.