Amosi 7:1-9
Amosi 7:1-9 BHN
Siku moja, Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono: Nilimwona Mungu anaumba nzige kundi zima, mara baada ya watu kumaliza kukata nyasi kwa ajili ya wanyama wa mfalme. Wakati huo, nyasi zilikuwa ndio zinaanza kuchipua tena. Niliwaona nzige hao wakila na kumaliza kila jani katika nchi. Ndipo nikasema: “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi utuhurumie! Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi? Wao ni wadogo mno!” Basi, Bwana Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake, akasema, “Haitakuwa hivyo!” Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono mengine: Nilimwona Bwana Mwenyezi-Mungu akiuita moto wa hukumu ya kuwaadhibu watu. Moto huo uliunguza vilindi vikuu vya bahari, ukaanza kuiteketeza nchi kavu. Ndipo nikasema: “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi uache kuadhibu! Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi? Wao ni wadogo mno!” Basi, Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake, akasema: “Hili pia halitatukia.” Mwenyezi-Mungu alinijalia tena maono mengine: Nilimwona Mwenyezi-Mungu amesimama karibu na ukuta, ameshika mkononi mwake uzi wenye timazi. Naye akaniuliza: “Amosi, unaona nini?” Nikamjibu, “Naona timazi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akasema: “Tazama! Naweka timazi kati ya watu wangu Waisraeli. Sitavumilia tena maovu yao. Huko vilimani ambako wazawa wa Isaka hutambikia, kutafanywa kuwa uharibifu mtupu na maskani ya Waisraeli yatakuwa magofu. Nitaushambulia kwa vita ukoo wa mfalme Yeroboamu.”