Kutoka 25:1-9
Kutoka 25:1-9 SRUV
BWANA akanena na Musa, akamwambia, Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii; dhahabu, fedha na shaba, na nyuzi rangi za buluu, zambarau na nyekundu, na nguo za kitani safi, na singa za mbuzi; na ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, na miti ya mjohoro, na mafuta ya ile taa, na viungo vya manukato kwa yale mafuta ya kupaka, na kwa ule uvumba wenye harufu nzuri; na vito vya shohamu, na vito vingine vya kutiwa kwa ile naivera, na kwa kile kifuko cha kifuani. Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao. Sawasawa na haya yote nikuoneshayo, mfano wa maskani, na mfano wa samani zake zote, ndivyo mtakavyovifanya.