Ayubu 42:10-17
Ayubu 42:10-17 SRUV
Kisha BWANA akamrejeshea Ayubu mali yake, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. Ndipo wakamwendea ndugu zake wote, wanaume kwa wanawake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakampa pole na kumliwaza kwa ajili ya mateso hayo yote aliyoleta BWANA juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja. Basi hivyo BWANA akaubariki huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo elfu kumi na nne, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu moja, na punda wake elfu moja. Tena alikuwa na watoto wa kiume saba, na binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi pamoja na ndugu zao wa kiume. Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia moja na arubaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hadi kizazi cha nne. Basi Ayubu akafa, akiwa mzee sana mwenye kujawa na siku.