Wafilipi 4:1-9
Wafilipi 4:1-9 SRUV
Basi, ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji langu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu. Namsihi Euodia, namsihi na Sintike, wawe na nia moja katika Bwana. Naam, nataka na wewe pia, mtumwa mwenzangu wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliofanya kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima. Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yuko karibu. Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya heshima, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.