Wafilipi 4:1-9
Wafilipi 4:1-9 BHN
Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, ninaotamani sana kuwaoneni, nyinyi mlio furaha yangu na taji ya ushindi wangu, ndivyo basi mnavyopaswa kukaa imara katika kuungana na Bwana, enyi wapenzi wangu. Euodia na Suntike, nawaombeni na kuwasihi mpatane kama ndugu katika Bwana. Nawe ndugu yangu mwaminifu, nakutaka uwasaidie akina mama hao, kwani wamefanya kazi ya kueneza Injili kwa bidii pamoja nami na Klementi na wafanyakazi wenzangu wengine wote ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uhai. Basi, furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: Furahini! Upole wenu ujulikane kwa watu wote. Bwana yu karibu. Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, zingatieni mambo mema na yanayostahili kusifiwa; mambo ya kweli na bora; mambo ya haki, safi, ya kupendeza na ya heshima. Tekelezeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu; mambo mliyosikia nimesema na kuona nimeyatenda. Naye Mungu anayetujalia amani atakuwa pamoja nanyi.