Zaburi 49:1-12
Zaburi 49:1-12 SRUV
Sikieni haya, enyi mataifa yote; Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani. Watu wakuu na watu wadogo wote pia, Tajiri na maskini wote pamoja. Kinywa changu kitanena hekima, Na fikira za moyo wangu zitakuwa za busara. Nitatega sikio langu nisikie mithali, Na kufumbua fumbo langu kwa kinubi. Kwa nini niogope wakati wa shida, Ubaya ukinizunguka miguuni pangu? Ambao wanazitumainia mali zao, Na kujisifia wingi wa utajiri wao; Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, Wala kumlipa Mungu fidia kwa ajili ya maisha yake, (Maana fidia ya nafsi zao ina gharama, Wala hawezi kuitoa hata milele;) ndipo aishi milele asilione kaburi. Naam, ataliona, hata wenye hekima hufa; Mpumbavu na mjinga hupotea pamoja, Na kuwaachia wengine mali zao. Makaburi ni nyumba zao hata milele, Maskani zao vizazi hata vizazi. Japo waliwahi kuyamiliki mashamba, Kwa majina yao wenyewe. Lakini mwanadamu hadumu katika heshima, Bali amefanana na wanyama wapoteao.