Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 9

9
1Naye Yesu aliwaambia, “Ninawaambia Ukweli: baadhi yenu mnaosimama hapa mtauona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu kabla ya kufa kwenu.”
Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya
(Mt 17:1-13; Lk 9:28-36)
2Baada ya siku sita, Yesu akamchukua Petro, Yakobo na Yohana na kuwaongoza hadi mlima mrefu wakiwa peke yao tu. Na mwonekano wa Yesu ulibadilika mbele yao. Huko Yesu akabadilika sura nyingine akiwa mbele yao. 3Mavazi yake yakiwa na mng'ao, na meupe kabisa kuliko mtu anavyoweza kufua nguo kwa sabuni na kuitakatisha. 4Huko Eliya na Musa pia wakawatokea, na Yesu alizungumza na manabii hao wawili.
5Petro akafungua kinywa chake na kumwambia Yesu, “Mwalimu, ni vyema tupo hapa. Tufanye basi vibanda vitatu; moja kwa ajili yako, moja kwa ajili ya Musa na moja kwa ajili ya Eliya.” 6Petro aliyasema haya kwa sababu hakujua aseme nini, kwa sababu yeye na wenzake walikuwa wamepata hofu.
7Ndipo wingu likaja na kuwafunika wote kwa kivuli chake. Na sauti ikatoka mawinguni, ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa. Msikilizeni yeye.”
8Ndipo ghafula walipokuwa wakiangalia huku na huko, hawakuona mtu yeyote akiwa pamoja nao isipokuwa Yesu peke yake.
9Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote kile walichokiona mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka katika wafu.
10Hivyo hawakuwaeleza wengine juu ya jambo lile bali walijadiliana miongoni mwao wenyewe juu ya maana ya “kufufuka kutoka kwa wafu.” 11Wakamwuliza Yesu, “kwa nini walimu wa sheria wanasema Eliya lazima aje kwanza?”
12Yesu akawaambia, “Ndiyo, Eliya atakuja kwanza#9:12 atakuja kwanza Ama atatangulia. kuja kuyaweka mambo yote sawa kama jinsi yalivyokuwa hapo mwanzo. Lakini kwa nini imeandikwa juu ya Mwana wa Adamu#9:12 Mwana wa Adamu Jina lingine alilojitambulisha Yesu. ya kwamba itampasa kuteswa na kudhalilishwa? 13Lakini ninawaambia, Eliya amekuja,#9:13 Eliya amekuja Habari hii inamhusu Yohana Mbatizaji. na walimtendea kila kitu walichotaka, kama vile ilivyoandikwa#9:13 kama vile ilivyoandikwa Hii inahusu maandiko ya Agano la Kale. kuhusu yeye.”
Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu
(Mt 17:14-20; Lk 9:37-43a)
14Wakati Yesu, Petro, Yakobo, na Yohana walipowafikia wanafunzi wengine, waliliona kundi kubwa la watu lililowazunguka na wakawaona walimu wa Sheria wakibishana nao. 15Mara tu watu wote walipomwona Yesu, walishangazwa, na wakakimbia kwenda kumsalimia.
16Akawauliza, “Mnabishana nao kitu gani?”
17Na mtu mmoja kundini alimjibu, “Mwalimu, nilimleta mwanangu kwako ili umponye. Yeye amefungwa na pepo mbaya anayemfanya asiweze kuzungumza. 18Na kila mara anapomshambulia humtupa chini ardhini. Naye hutokwa mapovu mdomoni na kusaga meno yake, huku akiwa mkakamavu. Nami niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze kutoka ndani yake, lakini hawakuweza.”
19Kisha Yesu akajibu na kuwaambia, “ninyi kizazi kisichoamini, kwa muda gani niwe pamoja nanyi? Kwa muda gani nitapaswa kuchukuliana nanyi? Mleteni huyo mvulana kwangu.”
20Wakamleta yule mvulana kwake. Na yule pepo alipomwona Yesu, kwa ghafula akamtingisha yule mvulana ambaye alianguka chini kwenye udongo, akivingirika na kutokwa povu mdomoni.
21Yesu akamwuliza babaye, “Kwa muda gani amekuwa katika hali hii?”
Yule babaye akajibu akisema, “amekuwa katika hali hii tangu utoto. 22Mara nyingi anamtupa katika moto ama katika maji ili kumwua. Lakini ikiwa unaweza kufanya kitu chochote, uwe na huruma na utusaidie.”
23Yesu akamwambia, “Una maana gani kusema ‘ikiwa unaweza’? Kila kitu kinawezekana kwake yeye anayeamini.”
24Mara, babaye yule mvulana alilia kwa sauti kubwa na kusema, “Naamini! Nisaidie kutokuamini kwangu.”
25Yesu alipoona lile kundi likizidi kuwa kubwa, alimkemea yule pepo mchafu na kumwambia, “Wewe pepo uliyemfanya mvulana huyu asiweze kusikia na asiweze kusema, nakuamuru, utoke ndani yake, na usimwingie tena!”
26Na pepo yule alilia kwa sauti, akamtupa yule mvulana chini katika mishituko ya kutisha, kisha akatoka, naye akawa kama mtu aliyekufa, kiasi kwamba watu wengi wakadhani ya kuwa amekufa. 27Lakini Yesu akamshika yule mvulana mikononi, na kumwinua naye akasimama.
28Baada ya Yesu kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuuliza wakiwa peke yao, “Kwa nini sisi hatukuweza kumfukuza pepo yule?”
29Naye akawaambia, “Aina hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa maombi.”#9:29 maombi Nakala zingine za Kiyunani zina “maombi na kufunga”.
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
(Mt 17:22-23; Lk 9:43-45)
30Wakaondoka mahali pale na kusafiri kupitia Galilaya. Yesu hakutaka mtu yeyote kujua walikuwa huko, 31alitaka kuwafundisha wanafunzi wake peke yake. Na Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kuwekwa mikononi mwa watu wengine, nao watamwua. Kisha siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.” 32Lakini hawakuuelewa usemi huu, na walikuwa wanaogopa kumuuliza zaidi.
Nani ni Mkuu Zaidi?
(Mt 18:1-5; Lk 9:46-48)
33Kisha wakaja Kapernaumu. Na Yesu alipokuwa ndani ya nyumba aliwauliza, “Je! mlikuwa mnajidiliana nini njiani?” 34Lakini wao walinyamaza kimya, kwa sababu njiani walikuwa wamebishana juu ya nani kati yao alikuwa ni mkuu zaidi.
35Hivyo Yesu aliketi chini, akawaita wale kumi na mbili, na akawaambia, “Ikiwa yupo mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, inapasa basi awe wa mwisho kuliko wote na mtumishi wa wote.”
36Akamchukua mtoto mdogo mikononi mwake na kumsimamisha mbele yao. Akimkumbatia mtoto huyo, Yesu alisema, 37“Yeyote atakayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu hapa kwa sababu ya jina langu basi ananikaribisha na mimi pia. Yeyote anayenikubali mimi hanikubali mimi tu bali anamkubali pia yeye aliyenituma.”
Yeyote Ambaye Hayuko Kinyume Chetu Yuko Pamoja Nasi
(Lk 9:49-50)
38Yohana akamwambia Yesu, “Mwalimu tulimwona mtu akifukuza pepo kwa jina lako. Nasi tulijaribu kumzuia, kwa sababu hakuwa mmoja wetu.”
39Lakini Yesu akawaambia, “Msimzuie, kwa sababu hakuna atendaye miujiza kwa jina langu kisha mara baada ya hilo aseme maneno mabaya juu yangu. 40Yeye ambaye hapingani na sisi basi yuko pamoja na sisi. 41Yeyote anayewapa ninyi kikombe cha maji kwa sababu ninyi ni wake Kristo.#9:41 Kristo Mpakwa mafuta au masihi, aliyechaguliwa na Mungu. Hakika ninawaambia ukweli kwamba, hatapoteza thawabu yake.
Yesu Aonya Kuhusu Chanzo cha Dhambi
(Mt 18:6-9; Lk 17:1-2)
42Yeyote anayemsababisha mmoja wa hawa walio wadogo ambao wananiamini mimi kujikwaa na kuanguka, itakuwa bora kwake ikiwa atatupwa baharini huku amefungwa jiwe la kusagia shingoni mwake. 43Ikiwa mkono wako unakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa na mkono mmoja kuliko kuwa na mikono miwili na kuenda Jehanamu, ambako kuna moto usiozimika. 44#9:44 Nakala zingine za Kiyunani zinaongeza mstari wa 44, ambao ni sawa na mstari 48. 45Na ikiwa mguu wako utakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa mlemavu kuliko kuwa na miguu miwili na kutupwa Jehanamu. 46#9:46 Nakala zingine za Kiyunani zinaongeza mstari wa 46, ambao ni sawa na mstari 48. 47Na kama jicho lako litakusababisha ufanye dhambi, liondoe. Ni bora uingie katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja kuliko kuwa nayo macho mawili na kutupwa Jehanamu, 48ambapo waliomo watatafunwa na funza wasiokufa na kuchomwa na moto usiozimika kamwe.#Isa 66:24
49Kwa kuwa kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.#9:49 Nakala zingine za Kiyunani zinaongeza, “Kila dhabihu itatiwa chumvi.” Katika Agano la Kale chumvi ilinyunyiziwa kwenye dhabihu. Mstari huu unaweza kuwa na maana kuwa wanafunzi wa Yesu watajaribiwa kwa mateso na kwamba wanapaswa kujitoa wenyewe kwa Mungu kama dhabihu.
50Chumvi ni njema. Lakini ikiwa chumvi itaharibika, utawezaje kuifanya chumvi tena? Muwe na chumvi miongoni mwenu na muishi kwa amani ninyi kwa ninyi.”

Iliyochaguliwa sasa

Marko 9: TKU

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia