2 Mose 16
16
Tombo na Mana.
1Walipoondoka Elimu, wakaingia wao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli katika nyika ya sini iliyoko katikati ya Elimu na Sinai siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili tangu hapo, walipotoka Misri. 2Huko nyikani wao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli wakamnung'unikia Mose na Haroni,#2 Mose 17:2. 3wakawaambia: Afadhali tungalikufa katika nchi ya Misri kwa kupigwa na mkono wa Bwana. Huko tulikaa na masufuria yenye nyama, tukapata vyakula vya kushiba, kwani mmetutoa huko na kutuleta huku nyikani, mwaue kwa njaa wao wote walio wa mkutano huu.#2 Mose 14:11.
4Ndipo, Bwana alipomwambia Mose: Mtaniona, nikiwanyeshea ninyi mvua ya mikate toka mbinguni, watu watoke tu kuiokota kila siku iipasayo hiyo siku, nipate kuwajaribu, kama wataendelea kuyashika maonyo yangu, au kama sivyo.#Yoh. 6:31; 1 Kor. 10:3. 5Lakini siku ya sita watakapotengeneza, waliyoiingiza, itakuwa ileile mara mbili, waliyoiokota siku zote. 6Kisha Mose na Haroni wakawaambia wana wote wa Isiraeli: Jioni na mjue, ya kuwa ndiye Bwana aliyewatoa ninyi katika nchi ya Misri. 7Tena asubuhi na mwuone utukufu wa Bwana, kwani amesikia, mlivyomnung'unikia yeye Bwana; maana sisi tu watu gani, mkitunung'unkia? 8Tena Mose akawaambia: Mtamjua Bwana hapo, atakapowapa leo jioni nyama za kula, tena asubuhi mikate ya kushiba, kwani Bwana amesikia, mlivyomnung'unikia yeye, maana sisi tu watu gani? Hamkutunung'unikia sisi, ila Bwana. 9Kisha Mose akamwambia Haroni: Waambie wao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli: Njoni kumtokea Bwana! Kwani ameyasikia manung'uniko yenu. 10Ikawa, Haroni aliposema nao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli, nao walipogeuka kutazama upande wa nyikani, mara utukufu wa Bwana ukatokea winguni.#4 Mose 12:5; 14:10; 16:19.
11Kisha Bwana akamwambia Mose kwamba: 12Nimeyasikia manung'uniko ya wana wa Isireli, sasa waambie kwamba: Saa za jioni mtakula nyama, tena asubuhi mtashiba mkate; ndipo, mtakapotambua, ya kuwa mimi Bwana ni Mungu wenu. 13Jioni tombo wakaja, wakayafunika makambi, tena asubuhi umande ulikuwa umeanguka kuyazunguka makambi.#4 Mose 11:31. 14Napo, umande uliokuwa umeanguka ulipoondoka, wakaona nyikani po pote punje ndogo sana zilizoviringana, nazo zilikuwa kama vitone vidogo vya umande juu ya nchi vilivyogandishwa na baridi. 15Wana wa Isiraeli walipoviona wakaulizana wao kwa wao: Man huu? ni kwamba: Nini hii? kwani hawakujua, kama ndio nini. Ndipo, Mose alipowaambia: Hiki ndicho kilaji, Bwana alichowapa ninyi kuwa chakula.#2 Mose 16:4. 16Nalo hili ndilo neno, Bwana aliloliagiza kwamba: Ziokoteni, kila mtu kama inavyompasa kula, vibaba viwili kwa kichwa kimoja! Sasa chukueni kila mtu kwa hesabu yao, alio nao hemani mwake! 17Wana wa Isiraeli wakafanya hivyo, wakaokota mmoja nyingi, mmoja chache, 18lakini walipopima kwa pishi, yule aliyeokota nyingi hakufurikiwa, wala aliyeokota chache hakupungukiwa, ila walikuwa wameokota kila mtu zilizompasa za kula.#2 Kor. 8:15. 19Kisha Mose akawaambia: Mtu asisaze za kesho!#Mat. 6:34; Luk. 11:3. 20Lakini hawakumsikia Mose, wengine wakasaza za kesho, zikapata funyo ndani, zikanuka vibaya. Naye Mose akawakasirikia. 21Hivyo wakaokota kila kulipokucha kila mtu zilizompasa za kula; lakini jua lilipowaka na ukali, zikayeyuka.
22Lakini walipookota siku ya sita, hivyo vilaji vilikuwa kipimo cha siku zote mara mbili, vibaba vinne mtu mmoja. Ndipo, wakuu wote wa mkutano walipokwenda kwa Mose kumpasha habari. 23Naye akawaambia: Hili ndilo, Bwana alilolisema kwamba: Kesho ni siku takatifu ya mapumziko ya kumpumzikia Bwana. Mnazotaka kuzikaanga zikaangeni! Mnazotaka kuzipika zipikeni! Zitakazosalia jiwekeeni za kungoja kesho!#1 Mose 2:2-3; 2 Mose 20:8. 24Walipoziweka za kesho, kama Mose alivyowaagiza, kuzikunuka vibaya, wala hazikupata funyo. 25Mose akawaambia: Zileni leo! Kwani leo ni siku ya mapumziko ya Bwana, leo hamtaziona nje nyikani. 26Siku sita mtaziokota, lakini siku ya saba ni ya mapumziko, haziko. 27Wengine walipotoka siku ya saba kuziokota, hawakuziona. 28Ndipo, Bwana alipomwambia Mose: Mpaka lini mtakataa kuyaangalia maagizo na maonyo yangu? 29Tazameni: Bwana amewapa ninyi siku ya mapumziko, kwa hiyo huwapa siku ya sita vilaji vya siku mbili. Kaeni tu kila mtu mahali pake, siku ya saba mtu asitoke hapo pake! 30Kwa sababu hii watu wakapumzika siku ya saba. 31Wao wa mlango wa Waisiraeli wakaziita jina lake: Mana; nazo zilikuwa nyeupe kama mbegu za mtama mweupe, napo walipozijaribu kula, zikawa tamu kama maandazi yaliyotiwa asali.
32Mose akasema: Hili ndilo neno, Bwana aliloliagiza: Jaza kisaga cha vibaba viwili mana, kiwekewe vizazi vyenu vijavyo, wapate kuviona vilaji hivi, nilivyowalisha ninyi nyikani nilipowatoa ninyi katika nchi ya Misri. 33Naye Mose akamwambia Haroni: Chukua kitungi kimoja, ukitie kisaga kimoja cha Mana, kisha kiweke mbele ya Bwana, kiwekewe vizazi vyenu vijavyo!#Ebr. 9:4. 34Kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, Haroni alivyokiweka mbele ya Sanduku la Ushahidi, kiangaliwe. 35Nao wana wa Isiraeli wakala Mana miaka 40, mpaka walipoingia katika nchi iliyokuwa yenye watu; hivyo ndivyo, walivyokula Mana, mpaka walipofika kwenye mipaka ya nchi ya Kanaani.#Yos. 5:12. 36Nacho kile kisaga kilipopimwa kwa mizani kilikuwa fungu la kumi la frasila.
Iliyochaguliwa sasa
2 Mose 16: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.