Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mose 3

3
Mungu anamtokea Mose huko Horebu.
1Mose alipokuwa akiwachunga mbuzi na kondoo wa mkwewe Yetoro aliyekuwa mtambikaji wa Midiani, akawapitisha mbuzi na kondoo katika hiyo nyika, afike kwenye mlima wa Mungu unaoitwa Horebu. 2Ndipo, malaika wa Bwana alipomtokea katika moto uliowaka kichakani katikati; naye alipotazama akaona: Kichaka hiki kinawaka moto kweli, lakini kichaka hiki hakiungui.#5 Mose 33:16; Tume. 7:30. 3Ndipo, Mose aliposema: Sharti niondoke, nifike hapo, nikione hiki kioja kikubwa, kama ni kwa sababu gani, kichaka hiki kisipoungua. 4Bwana alipomwona, alivyoondoka, apakaribie kutazama, ndipo, Mungu alipomwita toka hapo kichakani katikati na kusema: Mose! Mose! Akajibu: Mimi hapa! 5Naye akamwambia: Usifike hapa karibu! Vivue viatu vyako miguuni pako! Kwani mahali hapa, wewe unaposimama, ni nchi takatifu.#1 Mose 28:17; Yos. 5:15. 6Kisha akasema: Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Ndipo, Mose alipoufunika uso wake, kwani aliogopa kumwona Mungu.#Mat. 22:32. 7Naye Bwana akasema: Nimeyaona mateso yao walio ukoo wangu walioko Misri, nikasikia, wanavyonililia kwa ajili ya wasimamizi wao wakali, nikayajua maumivu yao.#2 Mose 2:23. 8Kwa hiyo nikashuka kuwaponya mikononi mwa Wamisri nikiwatoa katika nchi hiyo na kuwapeleka katika nchi iliyo njema na kubwa, nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali; ndiko, wanakokaa Wakanaani na Wahiti na Waamori na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi. 9Sasa kwa kuwa vilio vya wana wa Isiraeli vimefika kwangu, nikauona ukorofi, Wamisri wanaowatolea kwa kuwakorofisha, 10sasa nenda! Ninakutuma kwa Farao, uutoe ukoo wangu wa wana wa Isiraeli huko Misri. 11Lakini Mose akamwambia Mungu: Mimi ni nani nikienda kwa Farao, niwatoe wana wa Isiraeli huko Misri?#2 Mose 4:10; Yes. 6:5,8; Yer. 1:6. 12Akajibu: Kweli mimi nitakuwa na wewe. Nacho hiki na kiwe kielekezo chako, ya kuwa mimi Mungu nimekutuma: utakapowatoa watu hao huko Misri, mtanitumikia mimi huku mlimani. 13Mose akamwambia Mungu: Tazama! Nitakapofika kwa wana wa Isiraeli na kuwaambia: Mungu wa baba zenu amenituma kwenu, nao watakaponiuliza: Jina lake nani? nitawaambia nini? 14Ndipo, Mungu alipomwambia Mose: Nitakuwa niliyekuwa. Akasema: Hivi ndivyo, utakavyowaambia wana wa Isiraeli: Nitakuwa amenituma kwenu.#Ufu. 1:4,8. 15Tena Mungu akamwambia Mose: Hivi ndivyo, utakayowaambia wana wa Isiraeli: Bwana, Mungu wa baba zenu aliye Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu. Hili ni Jina langu kale na kale la kunikumbuka kwa vizazi na vizazi.#2 Mose 6:2-3; Yes. 42:8. 16Nenda tu, uwakusanye wazee wa Waisiraeli, uwaambie: Bwana, Mungu wa baba zenu, amenitokea, yeye aliye Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo, akaniambia: Nimewakagua ninyi, nikayaona mnayofanyiziwa huku Misri, 17nikasema: Nitawatoa ninyi katika mateso ya Misri na kuwapeleka katika nchi yao Wakanaani na Wahiti na Waamori na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi, nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali. 18Watakapoisikia sauti yako, utakwenda wewe pamoja na wazee wa Waisiraeli kwa mfalme wa Misri, umwambie: Bwana Mungu wa Waebureo amekutana nasi; kwa hiyo sasa tunataka kwenda nyikani safari ya siku tatu, tumtambikie Bwana Mungu wetu.#2 Mose 5:1,3. 19Lakini mimi ninajua, ya kuwa mfalme wa Misri hatawapa ruhusa kwenda zenu, isipokuwa kwa mkono wenye nguvu. 20Kwa hiyo nitaukunjua mkono wangu, niwapige Wamisri kwa matendo ya kustaajabisha, nitakayoyatenda katikati yao, baadaye atawapa ruhusa kwenda zenu. 21Lakini wao wa ukoo huu nitawapatia upendeleo machoni pao Wamisri, msiende mikono mitupu hapo, mtakapokwenda,#2 Mose 11:2-3; 12:35-36; 1 Mose 15:14. 22ila kila mwanamke na ajitakie kwa mwenyeji wake na kwa mwenzake wa kukaa naye katika nyumba moja vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu na nguo za kuwavika wana wenu wa kiume na wa kike. Hizi ndizo nyara, mtakazozichukua huko Misri.

Iliyochaguliwa sasa

2 Mose 3: SRB37

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia