Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mose 4

4
Mose anashindwa na Mungu.
1Mose akajibu kwamba: Lakini hawatanitegemea, wala hawataisikia sauti yangu, kwani watasema: Bwana hakukutokea. 2Ndipo, Bwana alipomwuliza: Mkononi mwako unashika nini? Akasema: Fimbo. 3Akamwambia: Itupe chini! Akaitupa chini; ndipo, ilipogeuka kuwa nyoka, naye Mose akamkimbia.#2 Mose 7:10. 4Lakini Bwana akamwambia Mose: Upeleke mkono wako, umkamate mkia! Akaupeleka mkono wake na kumkamata, akageuka kuwa fimbo tena mkononi mwake. 5Hivyo watakutegemea, kwamba amekutuma Bwana Mungu wa baba zao aliye Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. 6Kisha Bwana akamwambia tena: Upeleke mkono wako kifuani pako! Akaupeleka mkono wake kifuani pake; alipoutoa akauona mkono wake kuwa wenye ukoma uliong'aa kama chokaa juani. 7Kisha akamwambia: Urudishe mkono wako kifuani pako! Alipourudisha mkono wake kifuani pake na kuutoa kifuani pake akauona, ya kuwa umegeuka tena kuwa kama mwili wake. 8Itakapokuwa, wasikutegemee, wala wasiisikie sauti yako ukifanya kielekezo cha kwanza, wataitegemea sauti yako, utakapokifanya kielekezo cha pili. 9Lakini itakapokuwa, wasikutegemee, ijapo uvifanye vielekezo viwili, wala wasiisikie sauti yako, basi, chota maji mtoni, uyamwage pakavu! Ndipo, hayo maji, uliyoyachota mtoni, yatakapogeuka kuwa damu hapo pakavu.#2 Mose 7:17. 10Lakini Mose akamwambia Bwana: E Bwana wangu! Mimi si mtu ajuaye kusema tangu kale, wala tangu hapo, ulipoanza kusema na mtumishi wako, kwani kinywa changu ni kigumu, nao ulimu wangu ni mzito.#2 Mose 3:11; 6:12,30. 11Naye Bwana akamwambia: Aliyempa mtu kinywa ni nani? Au ni nani anayemweka mtu kuwa bubu au kiziwi au mwenye macho au kipofu? Si mimi Bwana?#Sh. 94:9. 12Sasa nenda! Nami nitakuwa na kinywa chako, nikufundishe utakayoyasema.#Mat. 10:19. 13Lakini akasema: E Bwana wangu! Tuma utakayemtuma na kumtumia! 14Ndipo, makali ya Bwana yalipomwakia Mose, akasema: Je? Mkubwa wako Haroni, yule Mlawi, hayuko? Simjui, ya kuwa anajua kabisa kusema? Naye utamwona, akikujia njiani, napo atakapokuona atafurahi moyoni mwake. 15Useme naye na kuyaweka haya maneno kinywani mwake! Nami nitakuwa na kinywa chako, tena na kinywa chake, niwafundishe ninyi mtakayoyafanya. 16Yeye ndiye atakayesema nao hao watu, awe kinywa chako, nawe wewe utakuwa kama Mungu wake.#2 Mose 7:1-2. 17Nayo fimbo hii uishike mkononi mwako ya kuvifanyizia vile vielekezo.
Mose anarudi Misri.
18Ndipo, Mose alipokwenda na kurudi kwake mkwewe Yetoro, akamwambia: Na niende kurudi kwa ndugu zangu walioko Misri, niwatazame, kama wako wazima bado. Yetoro akamwambia Mose: Nenda na kutengemana!#2 Mose 3:1. 19Kisha Bwana akamwambia Mose huko Midiani: Nenda kurudi Misri! Kwani wale watu walioitafuta roho yako wamekwisha kufa.#Mat. 2:20. 20Ndipo, Mose alipomchukua mkewe na wanawe, akawapandisha punda, akarudi katika nchi ya Misri; nayo ile fimbo ya Mungu Mose akaichukua mkononi mwake.#2 Mose 18:3-4. 21Naye Bwana akamwambia Mose: Hivyo, unavyokwenda kurudi Misri, viangalie vile vioja vyote, nilivyoviweka mkononi mwako, uvifanye mbele ya Farao! Lakini mimi nitaushupaza moyo wake, asiwape ruhusa hao watu kwenda zao.#2 Mose 7:3,13; 8:15,19,32; 9:12,35; 10:1,20,27; 14:4,17. 22Ndipo umwambie Farao: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Isiraeli ni mwanangu wa kuzaliwa wa kwanza.#Yer. 31:9; Hos. 11:1. 23Nami ninakuambia: Mpe mwanangu ruhusa, aende zake, apate kunitumikia! Lakini utakapokataa kumpa ruhusa utaniona mimi, nikimwua mwanao wa kuzaliwa wa kwanza.#4:23; 2 Mose 11:5; 12:29.
24Ikawa njiani, walipokuwa kituoni, Bwana akamjia akitaka kumwua.#1 Mose 17:14. 25Ndipo, Sipora alipokamata jiwe lenye makali, akalikata govi la mwanawe, akamgusa nayo miguu yake na kumwambia: Wewe u mchumba wangu aliyekombolewa kwa damu.#Yos. 5:2. 26Ndipo, alipomwacha; lakini hapo akamwita mchumba aliyekombolewa kwa damu kwa ajili ya kule kutahiri.
27Kisha Bwana akamwambia Haroni: Nenda nyikani kukutana na Mose! Alipokwenda akamkuta penye mlima wa Mungu, akamnonea. 28Mose akamsimulia Haroni maneno yote ya Bwana, aliyomtuma, navyo vielekezo vyote, alivyomwagiza. 29Kisha Mose na Haroni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa wana wa Isiraeli. 30Naye Haroni akayasema maneno yote, Bwana aliyomwambia Mose, navyo vile vielekezo akavifanya machoni pa watu. 31Ndipo, watu hao walipoyategemea yale maneno; nao waliposikia, ya kuwa Bwana amewakagua wana wa Isiraeli na kuyatazama mateso yao, wakainama na kumwangukia Mungu.#2 Mose 3:16.

Iliyochaguliwa sasa

2 Mose 4: SRB37

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia