Naye Bwana akasema: Nimeyaona mateso yao walio ukoo wangu walioko Misri, nikasikia, wanavyonililia kwa ajili ya wasimamizi wao wakali, nikayajua maumivu yao. Kwa hiyo nikashuka kuwaponya mikononi mwa Wamisri nikiwatoa katika nchi hiyo na kuwapeleka katika nchi iliyo njema na kubwa, nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali; ndiko, wanakokaa Wakanaani na Wahiti na Waamori na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi.