2 Mose 7
7
Mose na Haroni wanafanya vielekezo machoni pake Farao.
1Kisha Bwana akamwambia Mose: Tazama, nimekupa kuwa kama Mungu kwake Farao, naye kaka yako Haroni atakuwa mfumbuaji wako.#2 Mose 4:16. 2Wewe na uyaseme yote, nitakayokuagiza, naye kaka yako Haroni na amwambie Farao, awape wana wa Isiraeli ruhusa kutoka katika nchi yake. 3Lakini mimi nitaushupaza moyo wake Farao, nipate kufanya vielekezo na vioja vyangu vingi katika nchi ya Misri.#2 Mose 4:21. 4Farao asipowasikia ninyi, nitautokeza mkono wangu huko Misri; ndivyo, nitakavyowatoa vikosi vyangu walio ukoo wangu wa wana wa Isiraeli katika nchi ya Misri kwa mapatilizo makubwa. 5Wamisri nao watambue, ya kuwa Bwana ni mimi. Itakuwa hapo, nitakapowakunjulia Wamisri mkono wangu, nipate kuwatoa wana wa Isiraeli katikati yao.#2 Mose 8:22; 9:14,29. 6Mose na Haroni wakafanya, kama Bwana alivyowaagiza; hivyo ndivyo, walivyofanya. 7Mose alikuwa mwenye miaka 80, naye Haroni alikuwa mwenye miaka 83, waliposema Farao.
8Bwana akamwwambia Mose na Haroni kwamba:#2 Mose 4:3. 9Farao atakapowaambia: Fanyeni kioja, niwajue, mwambie Haroni: Ikamate fimbo yako, uitupe chini mbele ya Farao, iwe nyoka! 10Mose na Haroni walipofika kwake Farao wakafanya hivyo, kama Bwana alivyowaagiza: Haroni alipoitupa fimbo yake chini mbele yake Farao na mbele yao watumishi wake, ikawa nyoka. 11Ndipo, Farao naye alipowaita wajuzi na walozi, nao hao waganga wakafanya hivyo kwa uganga wao.#2 Mose 7:22; 8:7,18-19; 2 Tim. 3:8. 12Wakazitupa fimbo zao chini, kila mtu yake, nazo zikawa nyoka, lakini fimbo yake Haroni ikazimeza fimbo zao. 13Moyo wake Farao ukashupaa, asiwasikie, kama Bwana alivyosema.#2 Mose 4:21.
Pigo la kwanza: Maji yanageuka kuwa damu.
14Bwana akamwambia Mose: Moyo wa Farao ni mgumu, anakataa kuwapa watu hawa ruhusa kwenda zao. 15Kesho asubuhi nenda kwa Farao, utakapomwona, akitoka kwenda majini! Nawe simama hapo ukingoni kwa mto na kumngoja ukiishika mkononi mwako ile fimbo iliyogeuka kuwa nyoka! 16Nawe umwambie: Bwana Mungu wa Waebureo amenituma kwako kukuambia: Hao watu walio ukoo wangu wape ruhusa kwenda zao, wanitumikie nyikani! Lakini mpaka hapa hujasikia bado.#2 Mose 5:1. 17Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa hili na utambue, ya kuwa mimi ni Bwana: Tazama! Mimi nitakapoyapiga maji yaliyomo humu mtoni kwa fimbo hii, ninayoishika mkononi, ndipo, yatakapogeuka kuwa damu.#2 Mose 4:9. 18Nao samaki waliomo humu mtoni watakufa, nao mto utanuka vibaya, nao Wamisri watachukizwa kuyanywa maji ya mtoni. 19Kisha Bwana akamwambia Mose: Mwambie Haroni: Ichukue fimbo yako, kisha ukunjue mkono wako na kuuelekezea maji yao ya Misri yaliyomo vijitoni namo majitoni namo maziwani namo mashimoni, maji yanamokusanyika, yageuke kuwa damu! ndipo, yatakapogeuka kuwa damu katika nchi yote nzima ya Misri, nayo yaliyomo katika vyombo vya miti namo katika vyombo vya mawe.#Ufu. 11:6. 20Mose na Haroni wakafanya hivyo, kama Bwana alivyoagiza. Haroni alipoinyanyua hiyo fimbo na kuyapiga maji yaliyomo humo mtoni machoni pake Farao napo machoni pao watumishi wake, ndipo, maji yote yaliyomo humo mtoni yalipogeuzwa kuwa damu. 21Nao samaki waliokuwamo mtoni wakafa, nao mto ukanuka vibaya, Wamisri wasiweze kuyanywa hayo maji ya mtoni, maana yote yaligeuka kuwa damu katika nchi nzima ya Misri. 22Lakini waganga wa Misri wakavifanya nao kwa uganga wao; ndipo, moyo wake Farao uliposhupaa, asiwasikie, kama Bwana alivyosema.#2 Mose 7:11. 23Kisha Farao akageuka, akaingia nyumbani mwake, pasipo kuviweka moyoni mwake. 24Wamisri wote wakachimba maji pande zote za mtoni, wapate ya kunywa, kwani maji ya mtoni hawakuweza kuyanywa. 25Vikawa hivyo siku saba zote, Bwana alipokwisha kuupiga huo mto.
Iliyochaguliwa sasa
2 Mose 7: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.