Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mose 9

9
Pigo la tano: Kidei.
1Bwana akamwambia Mose: Nenda kwa Farao, umwambie: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Waebureo: Watu hawa walio ukoo wangu wape ruhusa kwenda zao, wanitumikie!#2 Mose 5:1. 2Lakini utakapokataa kuwapa ruhusa na kuwashika tena, 3ndipo, utakapouona mkono wa Bwana, ukiyajia makundi ya mashambani, farasi na punda na ngamia na ng'ombe na mbuzi na kondoo, wapatwe na kidei kikali sana.#2 Mose 3:20. 4Naye Bwana atayapambanua makundi ya Waisiraeli nayo makundi ya Wamisri, nao nyama wote pia walio wao Waisiraeli hatakufa hata mmoja wao. 5Bwana akaweka muda kwamba: Kesho Bwana atalifanya jambo hilo katika nchi hii. 6Kesho yake Bwana akalifanya kweli hilo jambo, wakafa nyama wa makundi yote ya Misri, lakini miongoni mwa makundi ya wana wa Isiraeli hakufa nyama hata mmoja. 7Farao alipotuma watu kutazama, wakaona, ya kuwa katika makundi ya Waisiraeli hakufa nyama hata mmoja. Lakini moyo wake Farao ukawa mgumu, hakuwapa hao watu ruhusa kwenda zao.#2 Mose 4:21.
Pigo la sita: Ndui.
8Bwana akamwambia Mose na Haroni: Jichukulieni majivu ya jikoni ya kuyajaza magao yenu! Kisha Mose ayasambaze juu angani machoni pake Farao. 9Ndipo, mavumbi yake membamba yatakapoieneza nchi yote ya Misri na kuwapata watu na nyama, watokewe na majipujipu ya ndui katika nchi yote ya Misri.#5 Mose 28:27. 10Ndipo, walipochukua majivu ya jikoni, wakaenda kusimama mbele ya Farao; ndipo, Mose alipoyasambaza juu angani, mara majipujipu ya ndui yakawatoka watu na nyama. 11Nao wale waganga hawakuweza kusimama mbele ya Mose kwa ajili ya hayo majipujipu, kwani hayo majipujibu yaliwapata wale waganga nao pamoja na Wamisri wote. 12Lakini Bwana akaushupaza moyo wa Farao, asiwasikie, kama Bwana alivyomwambia Mose.#2 Mose 4:21.
Pigo la saba: Mvua ya mawe.
13Bwana akamwambia Mose: Kesho asubuhi na mapema ujidamke, upate kumtokea Farao na kumwambia: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Waebureo: Watu hawa walio ukoo wangu wape ruhusa kwenda zao!#2 Mose 5:1. 14Kwani mara hii nitayatuma mapigo yangu yote, yakupate wewe moyoni mwako nao watumishi wako pamoja na watu wako, kusudi upate kujua, ya kuwa hakuna aliye kama mimi humu ulimwenguni mote. 15Kwani ningaliweza kuunyosha mkono wangu, ukupige wewe pamoja na watu wako kwa magonjwa yauayo, ukatoweka katika nchi hii; 16lakini nikikuweka, ni kwa sababu hiihii, nipate kukuonyesha nguvu zangu, Jina langu lipate kutangazwa katika nchi zote.#2 Mose 7:3; 14:14; Rom. 9:17. 17Ukiendelea kuwapingia wao walio ukoo wangu, usiwape ruhusa kwenda zao, 18utaniona, nikinyesha kesho saa zizi hizi mvua ya mawe mazito sana, isiyokuwa bado huku Misri yenye nguvu kama hiyo tangu siku ile, misingi yake ilipowekwa, hata sasa.#Iy. 38:22. 19Sasa tuma watu, wayahimize makundi yako nao wote wa kwako walioko mashambani kukimbilia nyumbani! Kwani watu wote, nao nyama wote watakaoonekana mashambani, wasiopelekwa nyumbani watakufa, mvua hiyo ya mawe itakapowanyeshea. 20Ndipo, wao walioliogopa hilo neno la Bwana miongoni mwa watumishi wa Farao walipowakimbiza watumwa wao na makundi yao na kuwingiza nyumbani. 21Lakini wasioliweka hilo neno la Bwana mioyoni mwao wakawaacha watumwa wao na makundi yao mashambani.
22Kisha Bwana akamwambia Mose: Unyoshe mkono wako na kuuelekeza mbinguni, mvua ya mawe inyeshe katika nchi yote ya Misri na kuwapiga watu na nyama na majani yote yaliyoko mashambani katika nchi ya Misri! 23Mose alipoiinua fimbo yake na kuielekeza mbinguni, ndipo, Bwana alipopiga ngurumo na kunyesha mvua ya mawe, moto wa umeme ukaanguka chini. Ndivyo, Bwana alivyonyesha mvua ya mawe katika nchi ya Misri.#Ufu. 16:21. 24Hiyo mvua ya mawe iliponyesha, moto ulichanganyika nayo hiyo mvua ya mawe mazito sana isiyokuwa bado katika nchi yote ya Misri yenye nguvu kama hiyo tangu hapo, watu walipoanza kukaa huko. 25Hiyo mvua ya mawe ikapiga katika nchi yote ya Misri yote pia yaliyokuwako mashambani, watu na nyama, nayo majani ya mashambani ikayapiga hiyo mvua ya mawe, ikaivunja nayo miti yote ya mashambani. 26Katika nchi ya Goseni tu, wana wa Isiraeli walikokaa, hiyo mvua ya mawe haikuwako. 27Ndipo, Farao alipotuma watu kumwita Mose na Haroni, akawaambia: Mara hii nimekosa; kwani Bwana ni mwongofu, lakini mimi na watu wangu tu wapotovu.#2 Mose 10:16. 28Niombeeni kwa Bwana, hizi ngurumo za Mungu zikome pamoja na mvua ya mawe kwa kuwa nyingi mno! Kisha nitawapa ninyi ruhusa kwenda zenu, msikae huku tena siku nyingi.#2 Mose 8:12. 29Naye Mose akamwambia: Nitakapotoka humu mjini nitamwinulia Bwana mikono yangu, ndipo, hizi ngurumo zitakapokoma, nayo hii mvua ya mawe haitakunya tena, kusudi mpate kujua, ya kuwa nchi ni yake Bwana. 30Lakini ninakujua wewe nao watumishi wako, ya kama hamjapata kumwogopa Bwana Mungu. 31Hivyo ndivyo, mipamba na miwele ilivyopigwa, kwani miwele ilikuwa imekwisha kuchanua, nayo mipamba ilikuwa imekwisha kuzaa. 32Lakini ngano na mtama hazikupigwa, kwa kuwa zilikuwa hazijaota bado. 33Mose alipotoka mle mjini mwake Farao, akamwinulia Bwana mikono yake; ndipo, ngurumo na mvua ya mawe zilipokoma, hata mvua haikunyesha tena katika nchi hiyo. 34Lakini Farao alipoona, ya kama mvua na mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akaendelea kukosa, akaushupaza moyo wake, yeye nao watumishi wake. 35Moyo wake Farao ukawa mgumu, asiwape wana wa Isiraeli ruhusa kwenda zao, kama Bwana alivyosema kinywani mwa Mose.#2 Mose 4:21.

Iliyochaguliwa sasa

2 Mose 9: SRB37

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia