Yohana 8
8
Mwanamke mzinzi.
1Yesu akaenda zake mlimani pa michekele. 2Asubuhi na mapema alipokuja tena Patakatifu, watu wote wakamwendea, naye akakaa akiwafundisha. 3Ndipo, waandishi na Mafariseo walipoleta mwanamke aliyefumaniwa katika ugoni, wakamsimamisha katikati. 4Kisha wakamwambia: Mfunzi, mwanamke huyu amefumaniwa papo hapo, alipofanya ugoni. 5Lakini Mose alituagiza katika Maonyo kuwaua wanawake walio hivyo kwa kuwapiga mawe; basi, wewe unasemaje?#3 Mose 20:10. 6Lakini walisema hivyo kwa kumjaribu, wapate neno la kumsuta. Yesu akainama chini, akaandika mchangani kwa kidole. 7Lakini walipokaza kumwuliza, akainua macho, akawaambia: Ninyi, asiye na kosa na aanze kumtupia jiwe! 8Kisha akainama tena akiandika mchangani.#Rom. 2:22. 9Nao walipoyasikia wakatoka mmojammoja, walioanza ndio wazee. Wakaachwa peke yao, yeye na yule mwanamke aliyekuwa hapo kati. 10Yesu alipoinua macho, akamwambia: Mama, wako wapi wale waliokusuta? Hakuna aliyekupatiliza? 11Aliposema: Hakuna, Bwana, Yesu akasema: Basi, hata mimi sikupatilizi; nenda zako! Lakini tangu sasa usikose tena!#Yoh. 5:14.
Kuwashinda Mafariseo.
12Kisha Yesu akawaambia tena akisema: Mimi ndio mwanga wa ulimwengu; anifuataye mimi hataendelea kwenda gizani, ila atakuwa anao mwanga wa uzima.#Yoh. 1:5,9; Yes. 49:6. 13Mafariseo wakamwambia: Wewe unajishuhudia mwenyewe; huu ushuhuda wako sio wa kweli. 14Yesu akajibu, akawaambia: Hata nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio wa kweli; kwani ninajua, nilikotoka, tena ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui, nitokako wala niendako.#Yoh. 5:31. 15Ninyi mwahukumu kimtu, mimi sihukumu mtu. 16Lakini ijapo nihukumu mtu, hukumu yangu ni ya kweli kwani siko peke yangu, ila tuko mimi na yule aliyenituma.#Yoh. 8:29. 17Hata katika Maonyo yenu imeandikwa: Ushuhuda wa watu wawili ni wa kweli.#5 Mose 19:15. 18Mimi ndiye ninayejishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia. 19Wakamwambia: Baba yako yuko wapi? Yesu akajibu: Hamnijui mimi, wala hammjui Baba yangu. Kama mngenijua mimi mngemjua naye Baba yangu.#Yoh. 14:7. 20Maneno haya aliyasema penye sanduku ya vipaji alipofundishia Patakatifu. Lakini hata mmoja hakumkamata, kwani saa yake ilikuwa haijafika.#Yoh. 7:30; Luk. 22:53.
Yesu atokako nako aendako.
21Akawaambia tena: Mimi nakwenda zangu, nanyi mtanitafuta, hata kufa mtakufa, mko katika ukosaji wenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kukufika.#Yoh. 7:34; 13:33. 22Wayuda wakasema: Je? Atajiua mwenyewe akisema: Niendako mimi, ninyi hamwezi kukufika?#Yoh. 7:35. 23Akawaambia: Ninyi mmetoka huku nchini, mimi nimetoka huko juu. Ninyi mmetoka humu ulimwenguni, mimi sikutoka humu ulimwenguni.#Yoh. 3:31. 24Kwa hiyo naliwaambia: Kufa mtakufa, mko katika ukosaji wenu. Kwani msiponitegemea, ya kuwa mimi ndiye, mtakufa, mko katika ukosaji wenu. 25Wakamwambia: Wewe ndiwe nani? Yesu akawaambia: Nimewaambia tangu mwanzo, kwa sababu gani niiseme tena? 26Kama ningeyasema yale mengi, mliyoyafanya, ningewaumbua; lakini aliyenituma ni wa kweli, nami niliyoyasikia kwake, ndiyo, ninayoyasema ulimwenguni. 27Hawakutambua, ya kuwa aliwaambia mambo ya Baba. 28Kisha Yesu akasema: Hapo, mtakapomkweza Mwana wa mtu, ndipo, mtakapotambua, ya kuwa mimi ndiye. Hakuna ninayoyafanya kwa mapenzi yangu, ila Baba aliyonifundisha ndiyo, ninayoyasema.#Yoh. 3:14; 12:32. 29Naye aliyenituma yuko pamoja nami; hakuniacha peke yangu, kwani mimi siku zote nayafanya, yanayompendeza.#Yoh. 8:16. 30Alipoyasema haya, wengi wakamtegemea.#Yoh. 7:31.
Uungwana wa kweli.
31*Hao Wayuda waliomtegemea Yesu akawaambia: Ninyi mkilikalia Neno langu, kweli m wanafunzi wangu,#Yoh. 15:14. 32mwitambue iliyo ya kweli, nayo iliyo ya kweli itawakomboa. 33Wakamjibu: Sisi tu uzao wake Aburahamu, hatujawa bado watumwa wa mtu, nawe wasemaje: Mtakombolewa?#Mat. 3:9. 34Yesu akawajibu: Kweli kweli nawaambiani: Kila afanyaye makosa ni mtumwa wa makosa.#Rom. 6:16,20; 1 Yoh. 3:8. 35Naye mtumwa hakai nyumbani kale na kale, lakini mwana ndiye akaaye kale na kale. 36Basi, huyo Mwana atakapowakomboa, mtakuwa mmekombolewa kweli.*#Rom. 6:18,22. 37Ninajua, ya kuwa ninyi m uzao wake Aburahamu. Lakini mnatafuta kuniua, kwani ndani yenu Neno langu halipati pa kukaa. 38Mimi niliyoyaona kwa Baba, ndiyo, ninayoyasema. Nanyi yafanyeni, mliyoyasikia kwake Baba! 39Ndipo, walipojibu na kumwambia: Baba yetu ni Aburahamu. Yesu akawaambia: Mkiwa watoto wake Aburahamu yafanyeni matendo yake Aburahamu! 40Lakini sasa mnatafuta kuniua; nami nimewaambia iliyo ya kweli, niliyoisikia kwa Mungu; hivyo Aburahamu hakuvifanya. 41Ninyi huyafanya matendo ya baba yenu. Wakamwambia: Sisi hatukuzaliwa kwa ugoni. Tunaye baba mmoja, ndiye Mungu. 42Yesu akawaambia: Mungu kama angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi. Kwani mimi nimetoka kwa Mungu, nikaja huku, lakini sikujijia mwenyewe tu, ila yeye alinituma. 43Mbona hamyatambui ninayoyasema? Ni kwa sababu hamwezi kulisikia Neno langu. 44Ninyi mmetoka kwa baba yenu, ni yule Msengenyaji; kwa hiyo mnataka kuzifanya tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa mwua watu tangu mwanzo, hakusimama penye kweli, kwani moyoni mwake hamna iliyo ya kweli. Anaposema uwongo anasema yaliyo yake yeye, kwani ni mwongo na baba yake uwongo.#1 Mose 3:4; 1 Petr. 5:8; 2 Petr. 2:4; 1 Yoh. 3:8-10. 45Lakini mimi ninaposema iliyo ya kweli, hamnitegemei.
46*Kwenu yuko nani anayeweza kuniumbua kuwa mwenye kosa lo lote? Nikisema iliyo ya kweli, mbona ninyi hamnitegemei?#2 Kor. 5:21; 1 Petr. 2:22; 1 Yoh. 3:5; Ebr. 4:15. 47Aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu. Kwa hiyo ninyi hamyasikii, kwani ninyi ham wa Mungu.#Yoh. 18:37; 1 Kor. 2:14. 48Wayuda wakajibu, wakamwambia: Sisi hatusemi kweli: Ndiwe Msamaria? Tena una pepo?#Yoh. 7:20. 49Yesu akajibu: Mimi sina pepo, ila ninamheshimu Baba yangu, nanyi mwanibeza. 50Lakini mimi sitafuti, nitukuzwe. Yuko anayevitafuta na kuhukumu.#Yoh. 5:41. 51Kweli kweli nawaambiani: Mtu atakapolishika Neno langu hataona kufa kale na kale.#Yoh. 6:40,47. 52Ndipo, Wayuda walipomwambia: Sasa tumekutambua, ya kuwa una pepo. Aburahamu amekufa, nao wafumbuaji wamekufa, na wewe wasema: Mtu atakapolishika Neno langu hataona kufa kale na kale? 53Je? Wewe u mkubwa kuliko baba yetu Aburahamu aliyekufa? Nao wafumbuaji wamekufa. Wajifanya kuwa nani? 54Yesu akajibu: Nikijipa utukufu mwenyewe, utukufu wangu ni wa bure; lakini Baba yangu ndiye anayenipa utukufu, ni yeye, mnayemsema ninyi: Ni Mungu wetu. 55Nanyi hamkumtambua yeye, lakini mimi nimemjua. Nami kama ningesema: Simjui, ningefanana nanyi kuwa mwongo. Lakini nimemjua, nalo Neno lake ninalishika.#Yoh. 7:28. 56Baba yenu Aburahamu alishangilia, kwamba aione siku yangu; akaiona, akafurahi. 57Wayuda wakamwambia: Hujapata bado miaka 50, nawe umemwona Aburahamu? 58Yesu akawaambia: Kweli kweli nawaambiani: Aburahamu alipokuwa hajakuwapo bado, mimi nilikuwa nipo.#Yoh. 1:1-2. 59Ndipo, walipookota mawe, wamtupie. Lakini Yesu akawa amefichika, akapatoka patakatifu.*#Yoh. 10:31.
Iliyochaguliwa sasa
Yohana 8: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.