Kutoka 25:31-40
Kutoka 25:31-40 BHN
“Utatengeneza kinara cha taa kwa dhahabu safi. Tako lake na ufito wa hicho kinara vitakuwa kitu kimoja, kadhalika na vikombe vyake, matumba yake na maua yake, vyote vitafuliwa kwa kipande kimoja tu cha dhahabu. Matawi sita yatatokeza kila upande wa ufito wake, matawi matatu upande mmoja na matawi matatu upande mwingine. Katika kila tawi kutakuwa na vikombe vitatu mfano wa maua ya mlozi, kila kimoja na tumba lake na ua lake. Na katika ufito kutakuwa na vikombe vinne mfano wa maua ya mlozi, pamoja na vifundo vyake na maua yake. Mahali panapotokezea kila jozi ya matawi yale sita, chini yake patakuwa na kifundo kimojakimoja. Vifundo hivyo na matawi yake yatakuwa kitu kimoja na kinara hicho, na chote kitafuliwa kwa dhahabu safi. Utatengeneza pia taa saba kwa ajili ya kinara hicho na kuziweka juu yake ili ziangaze kwa mbele. Tengeneza pia koleo zake na visahani vyake kwa dhahabu safi. Utatumia kilo thelathini na tano za dhahabu safi kutengeneza kinara hicho na vifaa vyake. Hakikisha kwamba umevitengeneza kwa mfano uliooneshwa kule mlimani.