Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 3:21-33

Maombolezo 3:21-33 BHN

Lakini nakumbuka jambo hili moja, nami ninalo tumaini: Kwamba fadhili za Mwenyezi-Mungu hazikomi, huruma zake hazina mwisho. Kila kunapokucha ni mpya kabisa, uaminifu wake ni mkuu mno. Mwenyezi-Mungu ndiye hazina yangu hivyo nitamwekea tumaini langu. Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wanaomtegemea, ni mwema kwa wote wanaomtafuta. Ni vema mtu kungojea kwa saburi ukombozi utokao kwa Mwenyezi-Mungu. Ni vema mtu kujifunza uvumilivu tangu wakati wa ujana wake. Heri kukaa peke na kimya, mazito yanapompata kutoka kwa Mungu. Yampasa kuinama na kujinyenyekesha, huenda ikawa tumaini bado lipo. Yampasa kumgeuzia shavu mwenye kumpiga, na kuwa tayari kupokea matusi yake. Mwenyezi-Mungu hatatutupa milele. Ingawa atufanya tuhuzunike, atakuwa na huruma tena kadiri ya wingi wa fadhili zake. Yeye hapendelei kuwatesa wala kuwahuzunisha wanadamu.