Mwanzo 17
17
Agano na kutahiriwa
1Wakati Abramu alipokuwa na umri wa miaka makumi tisa na tisa, Yawe akamutokea, akamwambia: “Mimi ni Mungu Mwenye Uwezo. Uendelee mbele yangu na kuwa mukamilifu. 2Nami nitafanya agano nawe na kuwazidisha wazao wako.” 3Abramu akaanguka uso mpaka chini. Naye Mungu akamwambia: 4“Ninafanya agano hili nawe: Utakuwa baba ya mataifa mengi. 5Tangu sasa, hautaitwa tena Abramu#17.5 Abramu: maana yake “baba aliyetukuzwa”., lakini utaitwa Abrahamu#17.5 Abrahamu: hapa linamaanisha “baba ya wengi”., maana nimekufanya kuwa baba ya mataifa mengi. 6Nitakufanya ukuwe na wazao wengi sana. Toka kwako nitatokeza mataifa mengi na wafalme.
7“Nitasimamisha agano langu nawe, wazao wako na vizazi vyao vyote milele; nitakuwa Mungu wako na Mungu wa wazao wako milele. 8Nitakupa wewe na wazao wako inchi hii ambamo unaishi kama mugeni. Ni kusema inchi yote ya Kanana ikuwe mali yenu milele; nami nitakuwa Mungu wao.”
9Kisha Mungu akamwambia Abrahamu: “Kwa upande wako, wewe utalishika agano langu, wewe peke yako, wazao wako na vizazi vyao vyote. 10Hivi ndivyo munavyopaswa kufanya wewe na wazao wako: kila mwanaume kati yenu anapaswa kutahiriwa. 11Mutatahiriwa kwa kukata magovi yenu na hiki kitakuwa ndicho kitambulisho cha agano kati yangu nanyi. 12-13Kila mutoto mwanaume kati yenu anapaswa kutahiriwa kwa umri wa siku nane. Vilevile watumwa waliozaliwa katika nyumba yenu au walionunuliwa kwa feza zenu kutoka kwa wageni wasiokuwa wa uzao wenu. Hiki ni kitambulisho cha agano langu katika miili yenu, agano la milele. 14Mwanaume yeyote asiyetahiriwa atatengwa na watu, maana atakuwa amevunja agano langu.”
Abrahamu anaahidiwa mutoto
15Kisha Mungu akamwambia Abrahamu: “Kuelekea muke wako, hautamwita tena jina lake Sarai, lakini jina lake litakuwa Sara. 16Nitamubariki, naye atakuzalia mutoto mwanaume. Nitamubariki Sara, naye atakuwa mama wa mataifa mengi na wafalme wa mataifa watatoka kwake.”
17Hapo Abrahamu akainama uso mpaka chini, akacheka ndani ya moyo wake akiwaza: “Itawezekana kweli mutoto kuzaliwa kwa muzee wa miaka mia moja? Na namna gani, Sara ambaye umri wake ni miaka makumi tisa, ataweza kupata mutoto?” 18Basi, Abrahamu akamwambia Mungu: “Ingekuwa heri ukubali ahadi hiyo yako imwelekee Isimaeli.”
19Mungu akamujibu: “Hapana. Muke wako Sara atakuzalia mutoto mwanaume, nawe utamwita Isaka#17.19 Isaka: maana yake ni: anacheka.. Nitaimarisha agano langu kwake na wazao wake, kuwa agano la milele.
20“Na juu ya Isimaeli, nimesikia ombi lako. Nitamubariki, nitamujalia watoto wengi na kuwazidisha sana. Isimaeli atakuwa baba wa watawala kumi na wawili, nami nitamufanya kuwa baba wa taifa kubwa. 21Lakini agano langu litasimama kwa Isaka ambaye Sara atakuzalia katika mwaka kwa wakati kama huu.” 22Basi, Mungu alipomaliza kuongea, akamwacha Abrahamu.
23Kisha Abrahamu akamutahiri mwana wake Isimaeli, na kuwatahiri watumwa wanaume wote waliozaliwa katika nyumba yake na walionunuliwa kwa feza zake. Aliwatahiri wote siku hiyohiyo kama vile Mungu alivyomwamuru. 24Abrahamu alikuwa na umri wa miaka makumi tisa na tisa alipotahiriwa. 25Na Isimaeli mwana wake alikuwa na umri wa miaka kumi na mitatu alipotahiriwa. 26Abrahamu na mwana wake Isimaeli 27pamoja na wanaume wote wa nyumba yake, watumwa wote waliozaliwa katika nyumba yake na wote walionunuliwa kwa feza zake walitahiriwa siku hiyohiyo.
Nke Ahọpụtara Ugbu A:
Mwanzo 17: SWC02
Mee ka ọ bụrụ isi
Kesaa
Mapịa
Ịchọrọ ka echekwaara gị ihe ndị gasị ị mere ka ha pụta ìhè ná ngwaọrụ gị niile? Debanye aha gị ma ọ bụ mee mbanye
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.