Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 20:1-17

Ezekieli 20:1-17 NEN

Katika mwaka wa saba, mwezi wa tano siku ya kumi, baadhi ya wazee wa Israeli wakaja ili kutaka ushauri kwa BWANA, wakaketi mbele yangu. Ndipo neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa nini mmekuja? Je, ni kutaka ushauri kwangu? Hakika kama niishivyo, sitawaruhusu mtake ushauri toka kwangu, asema BWANA Mwenyezi.’ “Je, utawahukumu? Je, mwanadamu, utawahukumu? Basi uwakabili kwa ajili ya machukizo ya baba zao na uwaambie: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Siku ile nilipochagua Israeli, niliwaapia wazao wa nyumba ya Yakobo kwa mkono ulioinuliwa nami nikajidhihirisha kwao huko Misri. Kwa mkono ulioinuliwa niliwaambia, “Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.” Siku ile niliwaapia wao kwamba nitawatoa katika nchi ya Misri na kuwaleta katika nchi niliyowachagulia, nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi nzuri kupita zote. Nami nikawaambia, “Kila mmoja wenu aondolee mbali sanamu za chukizo ambazo mmekazia macho, nanyi msijitie unajisi kwa sanamu za Misri. Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.” “ ‘Lakini waliniasi na hawakunisikiliza, hawakuondolea mbali sanamu za machukizo ambazo walikuwa wamezikazia macho, wala kuondolea mbali sanamu za Misri. Ndipo nikasema, nitawamwagia ghadhabu yangu na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko Misri. Lakini kwa ajili ya Jina langu nilifanya kile ambacho kingelifanya lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa waliyoishi miongoni mwao na ambao machoni pao nilikuwa nimejifunua kwa Waisraeli kwa kuwatoa katika nchi ya Misri. Kwa hiyo nikawaongoza watoke Misri na kuwaleta jangwani. Nikawapa amri zangu na kuwajulisha sheria zangu, kwa kuwa mtu anayezitii ataishi kwa hizo. Pia niliwapa Sabato zangu kama ishara kati yangu nao, ili wapate kujua kuwa Mimi BWANA niliwafanya kuwa watakatifu. “ ‘Lakini watu wa Israeli waliniasi Mimi jangwani. Hawakufuata amri zangu, bali walikataa sheria zangu, ingawa mtu yule anayezitii ataishi kwa hizo sheria, nao walizinajisi Sabato zangu kabisa. Hivyo nilisema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwaangamiza huko jangwani. Lakini kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile ambacho kitalifanya Jina langu lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli. Tena kwa mkono ulioinuliwa nikawaapia huko jangwani kwamba nisingewaingiza katika nchi niliyokuwa nimewapa, yaani, nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi nzuri kuliko zote, kwa sababu walikataa sheria zangu na hawakufuata amri zangu na wakazinajisi Sabato zangu. Kwa kuwa mioyo yao iliandama sanamu zao. Lakini niliwahurumia wala sikuwaangamiza wala hakuwafuta kabisa jangwani.