Ezekieli 20:1-17
Ezekieli 20:1-17 SRUV
Ikawa katika mwaka wa saba, mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja ili kuuliza kwa BWANA, wakaketi mbele yangu. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mmekuja kuniuliza neno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi. Je! Utawahukumu, mwanadamu, utawahukumu? Uwajulishe machukizo ya baba zao; uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile nilipochagua Israeli, na kuwainulia wazao wa nyumba ya Yakobo mkono wangu, na kujidhihirisha kwao katika nchi ya Misri, hapo nilipowainulia mkono wangu, nikisema, Mimi ni BWANA, Mungu wenu; katika siku ile niliwainulia mkono wangu, kuwatoa katika nchi ya Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyowapelelezea, itiririkayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote; nikawaambia, Kila mtu kwenu na atupilie mbali machukizo ya macho yake, wala msijitie unajisi kwa vinyago vya Misri, Mimi ni BWANA, Mungu wenu. Lakini waliniasi, wala hawakutaka kunisikiliza; hawakutupilia mbali kila mtu machukizo ya macho yake, wala hawakuviacha vinyago vya Misri; ndipo nikasema kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao, katikati ya nchi ya Misri. Lakini nilitenda kwa ajili ya jina langu, ili lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao walikaa pamoja nao, ambao machoni pao nilijidhihirisha kwao, kwa kuwatoa katika nchi ya Misri. Basi nikawatoa katika nchi ya Misri, nikawaleta jangwani. Nikawapa amri zangu, na kuwaonesha hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda. Tena niliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye. Lakini nyumba ya Israeli waliniasi jangwani; hawakuenda katika amri zangu, wakazikataa hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda; na sabato zangu walizitia unajisi sana; ndipo nikasema, Nitamwaga hasira yangu juu yao jangwani, ili niwaangamize. Lakini nilitenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi machoni pa mataifa, ambao niliwatoa mbele ya macho yao. Tena niliwainulia mkono wangu jangwani, ya kwamba sitawaingiza katika nchi ile niliyokuwa nimewapa, itiririkayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote; kwa sababu walizikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika amri zangu, wakazitia unajisi sabato zangu, kwa maana mioyo yao iliandama vinyago vyao. Walakini jicho langu likawahurumia nisiwaangamize kabisa, wala sikuwakomesha kabisa jangwani.