Ezekieli 20:1-17
Ezekieli 20:1-17 BHN
Mwaka wa saba tangu kuhamishwa kwetu, siku ya kumi ya mwezi wa tano, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja kumwuliza Mwenyezi-Mungu shauri, wakaketi mbele yangu. Basi, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu, sema na hao wazee wa Israeli. Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Je, mmekuja kuniuliza shauri? Hakika, kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nasema kuwa sitakubali kuulizwa kitu na nyinyi. “Wewe mtu, je, uko tayari kuwahukumu watu hawa? Basi, wahukumu. Wajulishe waliyofanya wazee wao. Waambie kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile nilipowachagua Waisraeli niliwaapia wazawa wa Yakobo. Nilijidhihirisha kwao nchini Misri, nikawaapia nikisema: Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Siku hiyo niliwaapia kwamba nitawatoa nchini Misri na kuwaongoza mpaka kwenye nchi niliyowachagulia, nchi inayotiririka maziwa na asali na nchi nzuri kuliko nchi zote. Niliwaambia: ‘Tupilieni mbali machukizo yote mnayoyapenda; msijitie unajisi kwa sanamu za miungu ya Misri, kwa maana mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.’ Lakini waliniasi, hawakutaka kunisikiliza. Hakuna hata mmoja wao aliyetupilia mbali machukizo yale waliyoyapenda, wala hawakuachana na sanamu za miungu ya Misri. Basi, nikafikiri kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuitimiza hasira yangu juu yao wakiwa kulekule nchini Misri. Lakini nilijizuia kufanya hivyo kwa heshima ya jina langu ili lisidharauliwe kati ya watu wa mataifa wanaoishi nao, hao walioona nikijijulisha kwa Waisraeli wakati wa kuwatoa katika nchi ya Misri. “Basi, mimi niliwatoa nchini Misri, nikawapeleka jangwani. Niliwapa kanuni zangu na kuwafundisha amri zangu ambazo mtu akizifuata huishi. Niliwapa pia Sabato zangu ziwe ishara kati yangu na wao, wapate kujua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu ninayewatakasa. Lakini Waisraeli waliniasi huko jangwani; hawakuzifuata kanuni zangu, bali walizikataa sheria zangu ambazo mtu akizifuata huishi. Sabato zangu walizikufuru daima, nami nikasema kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuwaangamiza hukohuko jangwani. Lakini nilijizuia kufanya hivyo kwa sababu ya heshima ya jina langu ili nisidharauliwe kati ya watu wa mataifa ambao walishuhudia jinsi nilivyowatoa Waisraeli nchini Misri. Hata hivyo, niliwaapia kulekule jangwani kwamba sitawaingiza katika nchi niliyowapa, nchi inayotiririka maziwa na asali na nchi nzuri kuliko nchi zote. Nilifanya hivyo kwa sababu walizikataa kanuni zangu na kuzikufuru Sabato zangu; kwani walipania kwa moyo sanamu za miungu yao. Lakini nilisalimisha maisha yao, sikuwaangamiza kule jangwani.