Ezekieli 21:1-17
Ezekieli 21:1-17 NEN
Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, uelekeze uso wako juu ya Yerusalemu na uhubiri dhidi ya mahali patakatifu. Tabiri dhidi ya nchi ya Israeli uiambie: ‘Hili ndilo BWANA asemalo: Mimi niko kinyume nawe. Nitautoa upanga wangu kwenye ala yake na kumkatilia mbali mwenye haki na mwovu. Kwa sababu nitamkatilia mbali mwenye haki na mwovu, upanga wangu utakuwa wazi dhidi ya kila mmoja kuanzia kusini mpaka kaskazini. Ndipo watu wote watajua ya kuwa Mimi BWANA nimeutoa upanga wangu kwenye ala yake, nao hautarudi humo tena.’ “Kwa hiyo lia kwa uchungu, mwanadamu! Lia kwa uchungu mbele yao kwa moyo uliopondeka na kwa huzuni nyingi. Nao watakapokuuliza, ‘Kwa nini unalia kwa uchungu?’ Utasema hivi, ‘Kwa sababu ya habari zinazokuja. Kila moyo utayeyuka na kila mkono utalegea, kila roho itazimia na kila goti litalegea kama maji.’ Habari hizo zinakuja! Hakika zitatokea, asema BWANA Mwenyezi.” Neno la BWANA likanijia, kusema: “Mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo Bwana asemalo: “ ‘Upanga, upanga, ulionolewa na kusuguliwa: umenolewa kwa ajili ya mauaji, umesuguliwa ili ungʼae kama umeme wa radi! “ ‘Je, tuifurahie fimbo ya utawala ya mwanangu Yuda? Upanga unaidharau kila fimbo ya namna hiyo. “ ‘Upanga umewekwa tayari ili kusuguliwa, ili upate kushikwa mkononi, umenolewa na kusuguliwa, umewekwa tayari kwa mkono wa muuaji. Piga kelele na uomboleze, ee mwanadamu, kwa kuwa upanga u dhidi ya watu wangu; u dhidi ya wakuu wote wa Israeli. Wametolewa wauawe kwa upanga pamoja na watu wangu. Kwa hiyo pigapiga kifua chako. “ ‘Kwa maana upanga huu umejaribiwa na kuhakikishwa, itakuwaje basi fimbo ya ufalme ya Yuda inayoudharau kama haitakuwepo tena, bali itakuwa imeondolewa kabisa? asema BWANA Mwenyezi.’ “Hivyo basi, mwanadamu, tabiri na ukapige makofi. Upanga wako na upige mara mbili, naam, hata mara tatu. Ni upanga wa kuchinja, upanga wa mauaji makuu, ukiwashambulia kutoka kila upande. Ili mioyo ipate kuyeyuka na wanaouawa wawe wengi, nimeweka upanga wa kuchinja kwenye malango yao yote. Lo! Umetengenezwa umetemete kama umeme wa radi, umeshikwa kwa ajili ya kuua. Ee upanga, kata upande wa kuume, kisha upande wa kushoto, mahali popote makali yako yatakapoelekezwa. Mimi nami nitapiga makofi, nayo ghadhabu yangu itapungua. Mimi BWANA nimesema.”